Wakulima wa parachichi nchini wamepata nafuu baada ya Taasisi ya Kudhibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) kutangaza usajili wa aina tano bora za miche ya zao hilo, hatua inayolenga kuongeza thamani na ushindani wa Tanzania katika soko la kimataifa.
Mkurugenzi Mkuu wa TOSCI, Nyasebwa Chimagu, alisema aina hizo ni Hass, Fuete, Pikatoni, Xikulu na Booth7, ambazo zinatajwa kustahimili magonjwa na kutoa mazao yenye kiwango bora kwa biashara.
Alibainisha kuwa kwa sasa Tanzania inashika nafasi ya tatu barani Afrika kwa uzalishaji wa parachichi, baada ya Afrika Kusini na Kenya, huku uzalishaji ukikadiriwa kufikia tani 198,000 kwa mwaka.

“Tunataka miche bora na iliyothibitishwa iwe msingi wa wakulima wetu ili kuongeza tija na kuiweka Tanzania kileleni mwa uzalishaji wa parachichi Afrika,” alisema Chimagu.
Aidha, TOSCI imetoa wito kwa wazalishaji wote wa miche kujisajili mapema ili kupata uhalali wa kisheria na kushiriki kikamilifu kwenye soko la kimataifa, huku baadhi ya waliokwisha sajiliwa wakieleza kuwa hatua hiyo imewapa nafasi ya kuongeza mapato na kupanua biashara zao.




