Katika moja ya matukio makubwa zaidi ya mwaka huu ya kibiashara, Kampuni ya Tanzania Breweries Plc (TBL), tawi la AB InBev na kiwanda kinachoongoza kwa kutengeneza bia nchini, imezindua Ripoti yake ya Uendelevu ya 2024 jijini Dar es Salaam Septemba 23, ikiwa na kauli mbiu “Grow, Brew, Sustain” (Kuongeza, Kutengeneza, Kudumisha).
Ripoti hiyo inathibitisha dhamira ya TBL kuendesha biashara kwa uwajibikaji, kulinda mazingira na kuchangia maendeleo ya kijamii. Pia inaonyesha mafanikio katika kupunguza hewa chafuzi, kukuza matumizi ya nishati jadidifu, kuhifadhi maji, kusaidia wakulima wa ndani na kulinda ustawi wa wafanyakazi. Hii inajumuisha taarifa ya mwaka mmoja, ikikamilisha Ripoti ya Ulimwengu ya AB InBev ya 2024 na kuonesha uongozi wa TBL katika kujenga biashara endelevu na thabiti.
Sifa kwa Uongozi wa Uwajibikaji
Balozi wa Ubelgiji nchini Tanzania, Peter Huyghebaert, ambaye alikuwa mgeni rasmi, aliipongeza TBL kwa kuonesha mfano bora katika uendeshaji biashara kwa uwajibikaji.







“Dhamira ya muda mrefu ya TBL katika ubora, ubunifu na uwajibikaji imeifanya kuwa moja ya kampuni kubwa na zenye heshima barani Afrika. Kwa kushikilia viwango vya kimataifa, inaathiri hata mifumo ya sekta nje ya Tanzania na kuonesha namna uwajibikaji wa kibiashara unavyoweza kuendesha maendeleo ya taifa, ustawi wa watu, sambamba na kukabiliana na changamoto kubwa ya wakati huu: mabadiliko ya tabianchi,” alisema.

Kurithisha Vizazi kwa Kuunganisha Asili na Mabadiliko
Mkurugenzi Mtendaji wa TBL, Michelle Kilpin, alisisitiza wajibu wa kampuni kwa vizazi vijavyo, akieleza hatua zilizopigwa katika kufanya tathmini ya hatari za maji, kupunguza hewa chafu kwenye mnyororo wa ugavi na utekelezaji wa vifungashio vinavyoweza kutumika tena, kwa kuendana na mkakati wa kimataifa wa AB InBev wa kupunguza kaboni.
“TBL imesimama kama kampuni inayoongoza utengenezaji bia nchini Tanzania, lakini zaidi ya kutengeneza na kuuza bia, tunatambua kuwa biashara yetu inategemea mazingira na jamii zinazotuzunguka. Ripoti hii tunayozindua leo inasimulia namna tunavyoishi kwa kuzingatia wajibu huo. Kile kinachotutofautisha siyo urithi wetu pekee, bali uwezo wetu wa kuunganisha asili na mageuzi,” alisema.







Vipengele Muhimu vya Ripoti ya 2024
- Uhifadhi wa maji: TBL imefanikiwa kufikia kiwango cha matumizi ya maji cha 2.73 hl/hl kwenye maeneo yenye changamoto kubwa za maji, huku zaidi ya asilimia 92 ya bidhaa zilizofungwa zikitengenezwa kwa vifaa vinavyoweza kurejelewa au kutumika tena.
- Kilimo endelevu: Kampuni imeshirikiana na zaidi ya wakulima 2,500 Kanda ya Kati na Kaskazini mwa Tanzania, wote wakiwa wamejumuishwa kifedha na kupata huduma za ugani ili kukuza kilimo endelevu na kuboresha maisha yao.
- Ukuaji shirikishi: Zaidi ya wafanyabiashara wadogo 25,000 wamewezeshwa kupata ujuzi wa kifedha, ushauri na teknolojia ili kuimarisha biashara zao kwenye mnyororo mzima wa thamani.
- Usalama kazini: TBL imeendelea kudumisha mazingira salama na jumuishi kazini, na hakuna kifo chochote kilichorekodiwa mwaka 2024, kutokana na kufuata kikamilifu kanuni za afya na usalama, mafunzo ya mara kwa mara na ukaguzi.
- Kampeni ya Ulevi wa Kistaarabu: Kupitia kampeni yake ya “Enjoy Like a Boss”, kwa kushirikiana na Shirika la Msalaba Mwekundu, TBL imefikia mamilioni ya Watanzania kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, ikihamasisha matumizi ya pombe kwa kiasi, uwajibikaji na usalama barabarani.








