Wastaafu mkoani Geita, wameeleza kufurahishwa kwao na maboresho yanayoendelea kutolewa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) hususan kujihakiki kwa kutumia simu janja kwani kunaokoa muda na kupunguza gharama.
Wameyasema hayo walipofika kujihakiki kwenye banda la PSSSF kwenye Maonesho ya 8 ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea katika viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan mjini Geita.
“Nimeelimishwa namna ya kutumia simu janja kujihakiki mimi mwenyewe nikiwa nyumbani, hii itasaidia kupunguza gharama kwa kusafiri kutoka Nyang’hwale kuja Geita mjini, lakini pia kunaokoa muda na kuniacha niendelee na shughuli zangu za uzalishaji,” alisema Jacob Andrew, ambaye ni mstaafu anayepokea pensheni PSSSF.



Mimi natoka Biharamulo, kwa mara ya kwanza leo nimejihakiki kidijitali kwa kutumia simu janja, mara nyingi huwa nahakikiwa kwa kutumia alama za vidole kwenye ofisi ya PSSSF Geita, hii itasaidia sana kupunguza gharama, alisema Mwesigwa Alex.
Naye Lucia Ezekiel, mstaafu kutoka Nyankumbu, ambaye anajishughulisha na biashara ndogondogo, alisema ameelekezwa hatua kwa hatua namna ya kujihakiki kwa kuyumia simu janja na ameelewa vizuri.
“ Kila mwaka ukifika wakati wa kujihakiki huwa naacha shughuli zangu na kulazimika kusafiri kuja Gerita mjini kujihakiki, kwa kutumia simu janja maana yake nikiwa na bando najihakiki mimi mwenyewe hapo hapo kwenye biashara yangu. Nawashukuru sana kwa elimu hii.” alisema Lucia.






