Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Samia Suluhu Hassan amesema ushindi mnono utakaopata chama hicho, Oktoba 29 wananchi ndio watakuwa mashahidi kutokana mwitikio mzuri wa mikutano yake ya hadhara.
Tangu Dk Samia azindue kampeni zake Agosti 28, 2025 jijini Dar es Salaam na kuendelea katika mikoa mingine, imeshuhudiwa maelfu wakihudhuria mikutano yake ya hadhara hali inayoashiria Watanzania wana muunga mkono na wana imani kubwa na mgombea huyo.
Dk Samia ameeleza hayo, leo Alhamisi Oktoba 16, 2025 akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Kaitaba mkoani Bukoba mkoni Kagera, akihitimisha ziara ya kampeni katika mkoa huo, kabla ya kwenda mikoa mingine ya magharibi.
“Kuna hadithi inasema kwa Waislamu, inasema watu ndio mashahidi wa Mungu, sasa watu waliotupokea kote kila tulipokwenda.Hawa ni mashahidi wa Mungu, kwamba Chama Cha Mapinduzi, kimefanya na kipo tayari kufanya na tukipata ushindi mnono hakuna wa kulalamika,”
“Watu wenyewe wametoka na kusema ‘yes’ (sawa), CCM imefanya kazi, sisi tunakiunga mkono Chama Cha Mapinduzi. Watu ni mashahidi wa Mungu, tunawashukuru sana…,” amesema Dkt Samia huku akishangiliwa na maelfu ya wananchi wa Mkoa wa Kagera.




