Afrika imeendelea kusisitiza hitaji la kuwepo kwa ufadhili wa uhakika, endelevu na wa kutosha katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Bara hilo limeonya kuwa bila rasilimali za kutosha na msaada wa kweli katika utekelezaji, maamuzi yanayopitishwa katika majukwaa ya kimataifa yataendelea kubaki kuwa ahadi na maneno matamu kwenye nyaraka, bila kuleta mabadiliko halisi kwa maisha ya mamilioni ya watu wanaoathirika.
Akizungumza kwa niaba ya nchi 54 wanachama wa Kundi la Wajadiliano wa Afrika (AGN) katika mkutano wa kufunga wa COP30 uliofanyika Belém, Brazil, Mwenyekiti wa AGN kutoka Tanzania, Dk. Richard Muyungi, alisisitiza kuwa Afrika inahitaji ufadhili wa kuaminika ili kubadilisha ahadi hizo kuwa hatua madhubuti za kimazingira.
“Licha ya hatua zilizopigwa katika Lengo la Kimataifa la Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi, ukosefu wa mifumo ya kifedha iliyo wazi na madhubuti unatishia kudhoofisha juhudi za Afrika za kulinda wananchi wake dhidi ya athari kali zinazozidi kuongezeka,” alisema Dk. Muyungi.




