Baada ya kusambaa kwa taarifa zinazodai kuwa Kocha Mkuu wa Simba SC, Fadlu Davis, ameondoka klabuni hapo pamoja na benchi lake la ufundi huku akibaki Kocha Msaidizi pekee, Selemani Matola, uongozi wa klabu hiyo umetuliza mashabiki wake.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, kupitia ukurasa wake wa Instagram ametoa wito kwa mashabiki wa Wekundu wa Msimbazi kuwa na subira, akisisitiza kuwa hakuna kitakachoharibika ndani ya timu hiyo.
Katika ujumbe wake, Ahmed aliandika:
“Good Morning Wana Simba. Tuendelee kuwa na subira tukisubiri taarifa sahihi na rasmi kutoka kwa viongozi wetu. Ninachoweza kuwahakikishia kwamba hakuna kitakachoharibika wala kurudi nyuma ndani ya klabu yetu.

Tunasonga mbele tukiwa bora na imara zaidi. Kwa sasa tutasikia mengi kila mtu akijaribu kupenyeza agenda zake kwa lengo la kuzua taharuki ndani ya klabu yetu. Jahazi letu lipo sawa, halijayumba wala kutikisika, tunaendelea na safari ya mafanikio.”
Simba SC kwa sasa inakabiliwa na michezo miwili muhimu: Septemba 25 itashuka dimbani kwenye uwanja wa KMC Complex kuvaana na Fountain Gate katika Ligi Kuu, kabla ya kurudiana na Gaborone United ya Botswana Septemba 28 kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa.
Licha ya kusafiri na timu kwenda Botswana na kushinda kwa bao 1-0 dhidi ya Gaborone United, kocha Fadlu Davis, msaidizi wake Darian Wilken pamoja na kocha wa makipa, Wayne Sandilands, hawakurejea nchini na kikosi hicho.
Taarifa zinaeleza kuwa benchi hilo la ufundi limepata ofa kubwa zaidi kutoka klabu ya Raja Athletic ya Morocco.