Nyota wa klabu ya Simba SC, Mohamed Bajaber, pamoja na kiungo wa Young Africans SC (Yanga), Duke Abuya, leo wameungana na wenzao katika mazoezi ya timu ya taifa ya Kenya, Harambee Stars, kujiandaa na michezo ya FIFA Series.
Wachezaji hao wawili wanaocheza soka lao katika Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara wameitwa kuimarisha kikosi cha Kenya kinachojiandaa na mechi za kimataifa za kirafiki chini ya dirisha la FIFA, linalolenga kuongeza ushindani na kuipa timu uzoefu zaidi wa kimataifa.
Mazoezi hayo yamefanyika katika hali ya ari kubwa huku benchi la ufundi likiwapima wachezaji wake kwa lengo la kupata kikosi bora kitakachowakilisha taifa hilo kwenye michezo hiyo muhimu. Bajaber na Abuya wameonyesha utayari mkubwa na morali ya hali ya juu, wakitarajiwa kuwa sehemu muhimu ya kikosi hicho.




Ushiriki wa nyota hao kutoka vilabu vya Tanzania ni ishara ya kuimarika kwa kiwango cha ligi ya ndani, huku pia ukionesha mchango wa klabu za Simba na Yanga katika kukuza vipaji vinavyotambulika kimataifa.
Harambee Stars inatarajiwa kutumia michezo ya FIFA Series kama sehemu ya maandalizi ya michuano mikubwa ijayo, huku ikilenga kupata matokeo chanya yatakayorejesha imani kwa mashabiki wa soka nchini Kenya.







