Katibu Mkuu mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Bashiru Ally amesema uongozi wa Mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho, Dkt Samia Suluhu Hassan utaendelea kukumbukwa kwa mambo matatu.
Ameyataka mambo hayo ni kufanikisha kukamilika kwa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, kuanzisha Tume ya Mipango na matarajio ya kuanzisha gridi ya taifa ya maji.
Dk Bashiru ametoa kauli hiyo leo, Jumatano Oktoba 8, 2025 alipozungumza katika mkutano wa kampeni za urais, wilayani Nyamagana, mkoani Mwanza.
“Tunamchagua Rais ambaye sio baada ya 2030 ataondoka, lakini ataondoka akituachia chombo cha mipango cha miaka 25 ijayo,” amesema.
Ameeleza hilo sio jambo dogo na aghalabu hutokea kwa nadra, kwani mkuu wan chi wa kwanza kuandaa mchakato wa dira ni Hayati Benjamin Mkapa na Dkt Samia anakuwa wa pili.
“Hata ukiwa Kizimkazi bado akili yako, alama yako, utashi wako, utakuwa unakumbukwa kupitia utashi huo na dira hiyo,” amesema.
Jambo lingine, amesema ni kuanzisha mchakato wa kuunda Tume ya Mipango na Gridi ya Taifa ya Maji, mambo ambayo yatabaki kuwa kumbukumbu za uongozi wake, hivyo anatakiwa achaguliwe tena ili aandike historia zaidi.




