Beki mpya wa Simba, Rushine De Reuck, aliyesajiliwa kutoka Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, ametajwa kuwa mchezaji wa kiwango cha juu na mwenye uwezo wa kucheza nafasi nne tofauti uwanjani — beki wa kati, kiungo mkabaji, beki wa kulia na kushoto.

Wachambuzi wa soka Afrika Kusini wamesifu usajili huo, wakieleza kuwa alikuwa akiwaniwa na Kaizer Chiefs na Orlando Pirates, lakini Sundowns walikataa kumuachia. Rushine mwenye miaka 29, aliwahi kung’ara chini ya Kocha Fadlu Davids akiwa Maritzburg United kabla ya kujiunga na Sundowns.
Mwandishi Fortunatus Kasomvi amesema De Reuck ni kiongozi mzuri, makini na hana historia ya makosa ya kizembe. Aidha, amepingana na madai ya kushuka kiwango, akisema kuchelewa kwake kucheza kulitokana na ushindani mkubwa wa wachezaji Sundowns, si kuporomoka kwa kiwango.
Mchambuzi mwingine, Mutotsi Dube, amesema De Reuck hakusumbuliwa na majeraha bali alikuwa nje kwa muda baada ya upasuaji wa meno. Simba imemsajili kwa mkataba wa mwaka mmoja na kipengele cha kuongeza mwaka mwingine.