Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) ambae ni mdhamini Mkuu wa Ligi Kuu ya NBC imesema licha ya mafanikio makubwa yanayoendelea kushuhudiwa katika ubora wa ligi hiyo hadi kuwa nafasi ya nne barani Afrika kwasasa bado dhamira ya benki hiyo ni kuhakikisha ligi hiyo inashika nafasi ya kwanza kwa ubora barani Afrika.

Dhamira ya benki hiyo iliwekwa wazi mwishoni mwa wiki na Mkuu wa Kitengo cha Fedha na Biashara wa benki hiyo Bw Joseph Lyuba wakati wa hafla fupi ya kuhitimisha rasmi kampeni yake yenye falsafa ya kimichezo ya ‘Shinda mechi zako Kinamna yako’ ambapo ilikabidhi zawadi ya gari aina ya BMW X1 kwa Bw Galus Peter Casto maruufu kama “Kweka”, mfanyabiashara mdogo ‘Machinga’ kwenye Soko la Kariakoo jijini Dar es salaama alieibuka mshindi wa kampeni hiyo.
Akizungumza kwenye hafla hiyo iliyofanyika kwenye tawi la benki hiyo Kariakoo Bw Lyuba alisema pamoja na kujivunia mafanikio ya ligi hiyo, benki hiyo ipo kwenye mkakati zaidi kuhakikisha kwamba inashirikiana na wadau zaidi ili kuongeza nguvu kwenye ligi hiyo lengo likiwa ni kuongeza hadhi ya ligi ya hiyo hadi kufikia nafasi ya kwanza barani Afrika.
“Mafanikio haya yanachochewa na ushirikiano mkubwa baina yetu kama wadhamini wakuu na wadau wenzetu wakiwemo Azam TV, wadau wote wa habari na mashabiki tukiongozwa na Shirikisho letu la Mpira wa miguu (TFF). Tunaamini mafanikio haya yatavutia wadau wengi zaidi na kwa pamoja tunakwenda kuifanya ligi hii kuwa namba barani Afrika,’’ alisema.
Akizungungumzia kampeni ya ‘Shinda mechi zako Kinamna yako’, Lyuba alisema ililenga kuchochea ukuaji wa uchumi miongoni mwa wateja wa benki hiyo kupitia uwekaji wa akiba.
“Tangu kuzinduliwa kwa kampeni hii inayotumia falsafa ya michezo kuboresha maisha ya wateja wetu mwezi Aprili mwaka jana tumweza kutoa zawadi za gari mbili aina BMW X1 kwa washindi wakuu pia tulitoa fursa kwa wateja hao kujishindia zawadi mbalimbali ikiwemo fedha taslimu, simu za mikononi, ‘laptops’, friji, ‘tablets’ za watoto, bima za afya pamoja na majiko ya kisasa ya kupikia.

Kwa mujibu wa Bw Lyuba jumla ya zawadi zenye thamani ya TSh milioni mia mbili zimetolewa kwa washindi mbalimbali wa kampeni hiyo tangu kuanzishwa kwake.
“Zaidi ya aina nane ya zawadi zilizotolewa kupitia kampeni hii zilikuwa zipo kimkakati zaidi tukilenga ziwasaidie wateja wetu kwenye kufanikisha majukumu yao kiuchumi ambayo ndio maana hali ya ‘Shinda mechi zako’ zikiwemo nyenzo za biashara na vitendea kazi vitakavyoweza kuwarahisishia kazi zao,’’ aliongeza.
Akifafanua zaidi kampeni hiyo Meneja Masoko wa Benki hiyo Bi Alina Kimaryo alisema ilihusisha wateja wote waliokidhi vigezo na masharti na wanaohudumiwa na benki hiyo kupitia huduma zake mbalimbali zikiwemo akaunti za Chanua, Akaunti ya Malengo, Akaunti ya Mwalimu pamoja na akaunti ya Johari.
“Mwisho wa kampeni hii ni mwanzo wa ujio wa kampeni nyingine nyingi kutoka NBC lengo ni kuunga mkono nia ya serikali ya kuchochea uchumi jumuishi kupitia uwekaji akiba kwenye taasisi rasmi za kifedha. Naendelea kuwasihi Watanzania wenzangu hususani vijana waendelee kutumia vema fursa za kampeni hizi ili waweze kunufaika kupitia malengo yake yaani kujiweka akiba huku pia wakiwa kwenye nafasi ya kujishidia zawadi mbalimbali’’ alisema.

Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa zawadi yake, Bw Kweka alieambatana na mke wake Bi Miriamu Kweka, pamoja na kuishukuru benki hiyo kwa makabidhiano hayo alisema ushindi huo umetokana na yeye kujiwekea akiba kupitia akaunti ya malengo kwa ajili ya ada za watoto wake lengo ambalo alifanikiwa kulitimiza.
“Nashukuru pamoja na kufanikiwa kulipa ada za watoto wangu kupitia akaunti ya malengo pia nimefanikiwa kupata zawadi ya gari litakalonisaidia kuwafikia zaidi wateja wangu huko mitaani. Nashukuru kwa kuwa zawadi hii itanirahisishia ‘Kushinda mechi zangu’’, alisema Bw Kweka. Kauli hiyo iliungwa mkono na mkewe ambae alitoa wito kwa wanawake wenzie nchini kuendelea kuwamasisha waume zao kujiwekea akiba kwenye taasisi rasmi za kifedha.
Akithibitisha uhalali wa kampeni hiyo Balozi wa Benki ya NBC, Bw Conrad Kennedy, maarifu kwa jina ‘Coy Mzungu’ alisema pamoja na kushuhudia uendeshwaji wa droo mbalimbali za kampeni hiyo pia alishuhudia uwepo wa maafisa wa kutoka Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania hatua iliyozidisha uwazi katika upatikanaji wa washindi hao.