Aliyekuwa nahodha wa Olympique de Marseille na raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Chancel Mbemba, ameifungulia kesi klabu yake ya zamani pamoja na raisi wake, akidai walimfanyia ukatili wa haki zake kama mchezaji kipindi alipoendelea kuwa klabuni hapo.
Mbemba, kupitia ripoti ya kesi iliyotolewa na gazeti la L’Equipe, alidai kwamba hakutendewa haki baada ya kuondolewa kwenye kikosi cha kwanza bila mazungumzo yoyote kati yake na uongozi wa klabu. Pia alieleza kuwa uongozi wa klabu ulizuia hata usajili wake alipojaribu kuondoka, lengo likiwa kumfanya akae bila kucheza. Kwa matokeo hayo, Mbemba alikaa mwaka mzima bila kucheza ligi kuu, akicheza tu kwenye timu ya taifa.
Kwa sasa, Chancel Mbemba amejiunga na LOSC Lille, klabu nyingine nchini Ufaransa. Kesi yake itapangiwa tarehe ya kusikilizwa hivi karibuni, na kama malalamiko yake yataonekana kuwa na mashiko, klabu ya Marseille inaweza kulipia fidia kulingana na maamuzi ya mahakama.