Monday, December 15, 2025
spot_img
HomeBiasharaDC Handeni awaonya maofisa mifugo matumizi mabaya ya vishikwambi

DC Handeni awaonya maofisa mifugo matumizi mabaya ya vishikwambi

Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Salum Nyamwese, amewataka maofisa mifugo wa Halmashauri ya Mji Handeni kutumia vishikwambi walivyokabidhiwa na serikali kwa kazi za kiofisi pekee na si kwa matumizi binafsi.

Akizungumza Septemba 22, 2025 wakati wa hafla ya kugawa vifaa hivyo mjini Handeni, Nyamwese alisema lengo la vishikwambi hivyo ni kuongeza ufanisi katika utendaji kazi na kusaidia harakati za utambuzi wa mifugo.

“Tusije tukasikia vinaingia kwenye matumizi ya mitandao ya kijamii kama ku-stream live, kuingia YouTube, Instagram au Facebook. Vishikwambi hivi vitumike kutekeleza majukumu yaliyokusudiwa,” alisema.

Aidha, alisisitiza vifaa hivyo vitunzwe ipasavyo na changamoto zozote ziwasilishwe Kitengo cha TEHAMA cha Halmashauri badala ya kupelekwa kwa mafundi wa mtaani.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Gerald Kauki, alisema hatua hiyo itawaongezea maofisa ufanisi katika kutoa huduma kwa wafugaji.

Naye Mkuu wa Divisheni ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Halmashauri hiyo, Aldegunda Matunda, alisema Halmashauri ina maofisa mifugo 27 wanaohudumia wafugaji 34,484 wenye mifugo zaidi ya 148,000.

Alifafanua kuwa katika mpango wa chanjo ya mifugo, Halmashauri imepokea vishikwambi 25 kutoka serikalini, ambapo awali walikuwa na viwili pekee.

“Utambuzi wa ng’ombe umefikia asilimia 58 na mbuzi asilimia 17. Tunaamini vifaa hivi vitachochea kasi ya utekelezaji wa mpango huo,” alisema.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments