Dk. Biteko ampongeza mwanafunzi aliyeeleza miradi ya umeme

Ā šŸ“ŒAmuahidi kutembelea mradi wa Julius Nyerere

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mheshimiwa Dkt. Doto Biteko, ameagiza mwanafunzi Mirabelle Msukari na wenzake kutoka Shule ya Msingi Sun Rise, wilayani Kinondoni, jijini Dar es Salaam, kufanyiwa ziara katika Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) ili kujifunza kwa vitendo namna umeme unavyozalishwa.

Mheshimiwa Biteko alitoa agizo hilo leo, Februari 18, kwa njia ya simu, baada ya Naibu Waziri wa Nishati, Mheshimiwa Judith Kapinga, kutembelea shule hiyo kwa lengo la kumpongeza Mirabelle. Mwanafunzi huyo alipata umaarufu kupitia mitandao ya kijamii baada ya kuonyesha uelewa mkubwa kuhusu miradi mbalimbali ya umeme inayoendelea nchini, ikiwemo JNHPP.

“Sisi tunakupongeza na tumefurahi kuona kwamba kwa umri wako unafuatilia masuala ya nishati. Sasa tutakupeleka kuliona Bwawa la Julius Nyerere ili uone jinsi umeme unavyozalishwa na kuendelea kujifunza zaidi. Tunatamani kukuona ukifanikiwa zaidi,” alisema Mheshimiwa Biteko.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Mheshimiwa Judith Kapinga, amesema kuwa miradi hii ya kimkakati inatekelezwa kwa jitihada za serikali chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ameonyesha dhamira ya dhati ya kuendeleza sekta ya umeme nchini.

“Wakati Mheshimiwa Rais anaingia madarakani, Mradi wa Julius Nyerere ulikuwa umefikia asilimia 33. Leo, tunavyozungumza, mradi huu umekamilika kwa zaidi ya asilimia 99, ambapo mashine nane tayari zimeingizwa kwenye gridi ya Taifa. Imebaki mashine moja pekee, na mradi uko mbioni kukamilika,” amesisitiza Kapinga.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano na Huduma kwa Wateja wa TANESCO, Irene Gowelle, akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), amesema kuwa wamepokea agizo la Dkt. Biteko na watahakikisha mwanafunzi huyo anafanya ziara katika mradi huo.

“Hatua hii inadhihirisha kuwa elimu na taarifa tunazotoa zinawafikia walengwa kwa usahihi, wakiwemo watoto. Mirabelle ametoa mfano mzuri wa jinsi elimu ya nishati inavyoweza kueleweka kwa urahisi,” amesema Gowelle.

Mbali na pongezi alizopokea, Mirabelle pia amepewa zawadi mbalimbali, ikiwemo kompyuta mpakato (laptop) na kiasi cha Shilingi Milioni Mbili.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *