Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Philip Mpango, amesisitiza umuhimu wa mifumo endelevu ya ufadhili na uzalishaji wa ndani wa vifaa vya matibabu ili kuhakikisha uthabiti wa kukabiliana na dharura za afya ya umma barani Afrika.
Kauli hiyo alitoa wakati akihutubia Mkutano wa Kamati ya Wakuu wa Nchi na Serikali wa Kituo cha Kudhibiti Magonjwa Afrika (Africa CDC), uliofanyika pembezoni mwa Kikao cha 80 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani.


Dk. Mpango alisema Tanzania imedhamiria kuongeza ukusanyaji wa rasilimali za ndani, kuimarisha masuluhisho ya kibunifu ya ufadhili, na kuunga mkono mipango ya kikanda inayopunguza utegemezi wa misaada kutoka nje.
Pia, alisisitiza uwekezaji katika viwanda vya ndani, ubia wa uhawilishaji teknolojia, na udhibiti wa pamoja barani Afrika ili kuimarisha uwezo wa kukabiliana na milipuko ya magonjwa ikiwemo Marburg na vimelea vingine vinavyoambukiza.


Aidha, alisisitiza umuhimu wa kuimarisha nguzo zote za dharura za afya ya umma, ikiwemo ufuatiliaji wa magonjwa, maabara, udhibiti wa maambukizi, vifaa, na uratibu wa dharura, pamoja na kushirikiana kati ya nchi wanachama wa Umoja wa Afrika, jumuiya za kiuchumi za kikanda, na Africa CDC.
Mkutano wa Kamati ya Africa CDC uliangazia masuala ya ufadhili endelevu wa sekta ya afya, uzalishaji wa ndani, na maandalizi dhidi ya milipuko ya maradhi, ukiwa chini ya kauli mbiu:
“Kuhakikisha Uhuru wa Afya Afrika: Uongozi wa Kisiasa kwa Ufadhili Endelevu wa Sekta ya Afya, Uzalishaji wa Ndani na Maandalizi Dhidi ya Milipuko ya Maradhi.”





