Mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan, ametembelea nyumbani kwa Rais mstaafu wa awamu ya pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi, leo Ijumaa Septemba 26, 2025, mjini Unguja, Zanzibar, kwa ajili ya kutoa pole kufuatia kifo cha mwanawe, Abbas Ali Mwinyi.
Abbas alifariki dunia jana Alhamisi, Septemba 25, 2025, katika Hospitali ya Lumumba, Unguja, alipokuwa akipatiwa matibabu. Marehemu anatarajiwa kuzikwa leo katika makaburi ya familia yaliyopo Mangapwani, Unguja.

Katika ziara hiyo ya faraja na mshikamano, Samia Suluhu aliungana na wanafamilia, ndugu, jamaa na marafiki wa karibu wa familia ya Mwinyi, akiwatia moyo katika kipindi hiki kigumu cha msiba.
Aidha, viongozi mbalimbali wa Serikali, chama na wananchi wameendelea kumiminika nyumbani kwa Rais mstaafu Mwinyi kutoa salamu za rambirambi na kushiriki maombolezo hayo.
Familia ya Mwinyi imemshukuru kila mmoja kwa sala, dua na mshikamano wanaoendelea kuonesha, huku ikiomba jamii kuendelea kuungana nao kwa sala na mshikamano wakati huu wa majonzi.




