Tuesday, December 9, 2025
spot_img
HomeHabariDk. Samia: Nichagueni nikamalizie kazi

Dk. Samia: Nichagueni nikamalizie kazi

Mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM),Dk. Samia Suluhu Hassan amewaomba Watanzania na wananchi wa mkoa wa Ruvuma kumchagua ili akakamilishe kazi za utekelezaji wa miradi ya maendeleo aliyoianza miaka mitano iliyopita.

Miongoni mwa miradi hiyo ni uboreshaji wa sekta za elimu,kilimo, umeme afya, maji na miundombinu ya barabara, akisema anakwenda kukamilisha ahadi hizo, kwa sababu ilani iliyopita ilipiga hatua katika utekelezaji wake.

Dk. Samia ameeleza hayo leo Jumapili Septemba 21,2025 wakati akiendelea kampeni zake za kusaka urais katika mikoa ya kusini akianzia wilayani Mbinga mkoani Ruvuma, baada ya kumaliza Unguja na Pemba.

“Septemba mwaka 2024, nilikuja katika ziara iliyokita kukagua miradi ya maendeleo, lakini mara hii nimekuja kivingine, nimekuja kuomba kura,”

“Nimekuja kwa kujiamini na ujasiri mkubwa kwamba miaka mitano iliyopita tumeweza na mitano inayokuja kwa uwezo wa Mungu, tutaweza,” amesema Dk. Samia huku akishangiliwa na wananchi wa Mbinga Mjini.

Akichambua sekta hizo, Dk. Samia amesema elimu, umeme na maji wanakwenda kuikamilisha miradi hiyo, kwa sababu hivi sasa imefikia hatua nzuri.

“Tuliambiwa umeme vijijini, sasa hivi tupo vitongoji, ukweli ni kwamba vitongoji nusu vya Tanzania vimeshaunganishwa.Sasa miaka mitano ijayo tunakwenda kuunganisha nusu iliyobaki ili kila Mtanzania apate,”

“Katika maji ukichukua kitaifa tunakaribia asilimia 90, tunapokwenda kimkoa, bado kuna mingine ipo nyuma, hivyo tuna kazi ya kufanya ili kumalizia,” amesema Dk. Samia.

Katika maelezo yake, Dk. Samia amesema anatambua Mbinga kuna maeneo maji hayajafika, lakini amewatoa hofu wakazi wa wilaya, akisema kuna miradi 21 itakayotekelezwa ili kumaliza changamoto hiyo.

Kuhusu afya na elimu, Dk. Samia amesema sekta hizo zitakuwa ndio kazi kila awamu itakayoingia kuongoza Serikali ikiwemo kujenga shule na hospitali, sambamba na kuhakikisha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba.

“Katika kilimo, Samia nawapongeza Mbinga kwa uzalishaji wa chakula, niwaahidi Serikali itaendelea kutoa ruzuku ya pembejeo na mbolea. Kwa ufugaji ruzuku ya chanjo ya mifugo itatolewa na huduma za ugani,” amesema Dk. Samia.

Dk. Samia amewaahidi wananchi wa Mbinga kuwa Serikali itaimarisha masoko ya mazao yao na kuwatafutia bei bora ili wakulima wanufuaike na jasho lao.

“Tutakwenda kujenga barabara ya Kitai, lakini pia tutazijenga zingine zipitike wakati wote, iwe mvua au jua,”

“Ahadi yetu ni kuwatumikia, ndio maana tunasema ‘kazi na utu, tunasonga mbele’ Sasa ndugu zangu, baada ya kueleza haya na ahadi nilizosikia na shamrashamra, hivi CCM inashindwaje hapa Mbinga, itashindwa kweli,”amehoji Dkt Samia na kujibiwa aah wapi.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments