Mgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Samia Suluhu Hassan amesema dhamira ya Serikali yake katika miaka mitano ijayo ni kumwezesha kila mwananchi kiuchumi kwa kuchukua hatua mbalimbali zitakazolifanikisha hilo.
Miongoni mwa hatua hizo kwa mujibu wa Dkt Samia, ni kujenga masoko na stendi katika maeneo mbalimbali, zitakazotumika na wananchi kufanya biashara na hatimaye kujipatia kipato.
Dkt Samia ametoa ahadi hiyo leo, Alhamisi Oktoba 9, 2025 alipozungumza na wananchi wa Musoma mkoani Mara, katika mkutano wake wa kampeni za urais.
Jambo lingine aliloahidi kulifanya kumwezesha mwananchi kiuchumi ni kutenga Sh200 bilioni kwa ajili ya uwezeshaji wa biashara ndogondogo ili zikue nao wajipatia kipato na kuimarisha ustawi wao.
Sio hayo tu, Dkt Samia amesema katika miaka mitano hiyo, atarasimisha biashara zisizo rasmi, ili wafanyabiashara wake wapate haki, fursa na neema zote kama wanazozipata wengine na kukuza vipato vyao.
Utoaji wa ruzuku ya mbolea, chanjo kwa mifugo ni mambo mengine aliyoyaahidi Dkt Samia ili kumwezesha mwananchi kiuchumi na kuimarisha vipato vyao.