Friday, November 14, 2025
spot_img
HomeHabariWananchi Itilima wapongeza mfumo wa malipo ya madhara wanyamapori

Wananchi Itilima wapongeza mfumo wa malipo ya madhara wanyamapori

Wananchi wa vijiji vya Nyantugutu, Lung’wa na Nding’ho wilayani Itilima, mkoani Simiyu, wameipongeza Serikali kwa kuunda na kuboresha mfumo wa ukusanyaji wa taarifa za wanyamapori wakali na waharibifu (Problem Animal Information System – PAIS), ambao umeharakisha na kurahisisha malipo ya kifuta jasho/machozi kwa waathirika wa madhara yanayosababishwa na wanyamapori.

Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Nding’ho, Salome Kambona, alisema hayo leo, Oktoba 9, 2025, katika mkutano wa hadhara wa kuelimisha wananchi kuhusu namna ya kukabiliana na changamoto za wanyamapori wakali na waharibifu uliofanyika kijijini humo.

“Tunaishukuru Serikali kwa mfumo huu ambao umeondoa ucheleweshaji wa malipo. Sasa ndani ya siku saba baada ya kutoa taarifa ya tukio la uharibifu, mwananchi analipwa fidia kupitia mfumo wa PAIS,” alisema Bi. Salome.

Mkazi wa Kijiji cha Nyantugutu, Mosses Saguda, naye alieleza kuwa mfumo huo mpya umepunguza urasimu uliokuwapo awali na kuleta unafuu mkubwa kwa wananchi.

“Tunaishukuru Serikali kwa utaratibu huu mpya wa kifuta jasho/machozi. Sasa tunalipwa moja kwa moja kupitia simu au benki, tofauti na zamani tulivyokuwa tunasubiri hadi mwaka mzima bila kulipwa,” alisema Bw. Saguda.

Hata hivyo, aliiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kulipa fidia kwa wananchi wanaoharibiwa mazao yao wakiwa tayari wameyahifadhi ghalani.

Akizungumza katika mkutano huo, Afisa Wanyamapori Mkuu kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Nassoro Wawa, alisema Serikali inatarajia wananchi waliopata elimu hiyo wataweza kukabiliana ipasavyo na wanyamapori wakali na waharibifu, pamoja na kufahamu sheria, kanuni na taratibu za umiliki wa nyara za Serikali.

“Nimewaeleza wananchi kuwa sheria zinaruhusu kuwekeza katika sekta ya wanyamapori, ikiwemo kuanzisha bucha, bustani, mashamba na ranchi za wanyamapori ili kujipatia kipato halali,” alisisitiza Bw. Wawa.

Elimu hiyo imetolewa kufuatia ongezeko la matukio ya wanyamapori wakali na waharibifu, hususan tembo, fisi, mamba na viboko, ambao wamekuwa wakisababisha uharibifu wa mazao na mali za wananchi katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Simiyu.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments