Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Samia Suluhu Hassan ameahidi ujenzi wa kiwanja cha ndege katika Mji wa Mugumu wilayani Serengeti ili kukuza na kurahisisha shughuli za utalii.
Amesema ahadi hiyo ipo katika Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2025/30, akisema hatua hiyo itawezesha watalii kutua moja kwa moja katika Mji wa Mugumu.
Dk Samia ameeleza hayo leo Ijumaa Oktoba 10,2025 katika mkutano wa hadhara wa kampeni eneo la Mugumu wilayani Serengeti mkoani Mara, wakati akihitimisha ziara ya kampeni mkoani humo kabla ya kutua Simiyu kwa mara nyingine.
Amefafanua kuwa Mugumu ni mji wenye umuhimu kwa fursa za uwekezaji wa hoteli za kitalii kwa sababu upo katikati ya hifadhi ya Serengeti na maeneo yaliyohifadhiwa kwa wageni wanatoka Sirari kwenda Kogatende eneo lenye utalii wa mzunguko wa nyumbu wanaohama kwenye ikolojia.
“Ni mji wa kimkakati wa utalii, kipindi hiki tumeshahudia uwekezaji mkubwa katika Mji wa Mugumu. Sasa ndani ya miaka mitano inayokuja, mkitupa ridhaa lengo letu ni kuendelea kutangaza vivutio vyetu ili kufikia watalii milioni 8 kwa mwaka ifikapo 2030.
“Hifadhi ya Taifa ya Serengeti itakuwa sehemu muhimu ya kufikisha watalii milioni 8, lakini katika ilani yetu tumewaahidi hapa Mugumu tutakuja kujenga kiwanja cha ndege, ipo katika ilani,” amesema Dk Samia.
Ahimizi umoja, mshikamano
Katika mkutano huo, Dkt Samia amesema pamoja na kuwepo kwa mila na desturi, suala la umoja wa Watanzania ni muhimu sana, akiwataka wananchi Serengereti kutambua kuwa maendeleo yanaweza kuletwa hata viongozi wanawake.
“Nimesema haya kwa sababu nimesikia maneno kuwa mgombea wetu (ubunge-Serengeti) ni mwanamke hivyo kwa mila na desturi zenu, hamtaki mwanamke, kwenye maendeleo hakuna mwanamke wala mwanaume,”
“Mimi ninayesema hapa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ndani ya miaka minne nimefanya mambo makubwa sana…sasa ingekuwa mwanamke hawezi, nisingeweza kuyafanya. Mungu ametuumba wote na akili sawa, akatupa na uwezo wa kufikiria,” amesema
Dk. Samia ambaye ni Mwenyekiti wa CCM, amefafanua kuwa mwanamke ndiye mtendaji mzuri na mwaminifu zaidi kwa sababu ya uoga kuliko mwanaume.
“Nataka niwaambie ndugu zangu, wazee wetu pamoja na mila na desturi zetu, maana nimeanza kusikia pia maneno kwamba huko CCM, Mara wametupa wagombea wanne wanawake, kwani wanawake wana nini?
“Niwaambie wanawake watachapa kazi sawasawa na wengine walivyochapa kazi, mkoa huu huu utaendelezwa na wanawake na wanaume kwa mshikamano,”
Dk Samia ameongeza kuwa, “Tanzania hii itajenga na kuendelezwa na wanawake na wanaume wote kwa umoja wetu, cha muhimu sote ni Watanzania, sote wa Taifa moja, sote lazima tushikamane kama waasisi wetu walivyotuambia tujenge nchi