📌Mgodi umeajiri Watanzania Asilimia 99
📌Asilimia 70 ni kampuni za Kitanzania zinazotoa huduma na bidhaa mgodini
📍Chunya
Chunya, Oktoba 2025 — Upanuzi wa shughuli za uchimbaji katika eneo la Porcupine North umeongeza muda wa uhai wa Mgodi wa Shanta Gold – New Luika kwa miaka mitano zaidi, kutoka mwaka 2029 hadi 2034, huku kampuni hiyo ikiendelea na tafiti za kuongeza uzalishaji wa dhahabu katika maeneo mengine.
Akizungumza na timu ya Madini Diary iliyotembelea mgodini hapo, Kaimu Meneja Mkuu wa Shanta Gold – New Luika, Mhandisi Ladislaus Kwesigabo, alisema shughuli za uzalishaji zinaendelea vizuri na kampuni inaendelea kufanya tafiti zaidi chini ya leseni nyingine inazomiliki, ili kuongeza uhai wa mgodi huo.


“Kupitia tafiti hizi na upanuzi wa Porcupine North, tunatarajia kuendeleza uzalishaji wa dhahabu kwa miaka zaidi na kuongeza mchango wa mgodi kwa uchumi wa taifa,” alisema Kwesigabo.
Mnamo Aprili 3, 2025, Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, alizindua rasmi shughuli za uchimbaji katika Porcupine North, eneo lililorejeshwa Serikalini baada ya mchakato wa kisheria kukamilika, kabla ya kumpata mwekezaji mpya — Shanta Mining Company Limited, kampuni ya Kitanzania iliyoanzishwa mwaka 2001.
Shanta ilianza uzalishaji wa dhahabu mwaka 2012, na tangu wakati huo imekuwa ikizalisha kati ya wakia 55,000 hadi 60,000 kwa mwaka. Mgodi huu umeajiri Watanzania kwa asilimia 99, ambapo asilimia 40 wanatoka maeneo yanayozunguka mgodi na asilimia 60 maeneo mengine ya nchi. Zaidi ya asilimia 70 ya kampuni zinazohudumia mgodi ni kampuni za Kitanzania.




“Fursa za kutoa huduma zipo wazi kwa wote wanaofuata taratibu. Tunahakikisha uwazi na uhalali katika zabuni na mikataba yetu,” aliongeza Kwesigabo.
Aidha, alisema mgodi huo umetoa nafasi nyingi kwa wanawake katika sekta za uhandisi, utafiti, uendeshaji mitambo na menejimenti, sambamba na kuwekeza kwenye huduma za kijamii ikiwemo afya, elimu, maji, kilimo, na miradi ya kuwaandaa wananchi kunufaika baada ya mgodi kufungwa.
Akizungumzia uchimbaji mdogo, alisema umeongezeka kwa kasi katika Wilaya ya Chunya kutokana na kuimarika kwa bei ya dhahabu, huku akitoa wito kwa wachimbaji wadogo kufuata sheria na kuepuka kuingilia leseni za wengine.
Kwa sasa, Shanta Gold inatekeleza shughuli zake katika maeneo yanayoshikana kati ya Mkoa wa Songwe na Mbeya (Chunya), ambapo mtambo wa kuchenjua dhahabu upo Songwe, na eneo jipya la Porcupine North liko Chunya. Kampuni hiyo pia inamiliki Mgodi wa Singida Gold Mine mkoani Singida.





