Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt Samia Suluhu Hassan amesema Serikali yake katika miaka mitano ijayo, itajenga soko la kisasa wilayani Mwanga, Mkoa wa Kilimanjaro, ili kuwasaidia wakulima kuuza bidhaa zao.
Dkt Samia ametoa kauli hiyo leo, Jumanne Septemba 30, 2025 alipozungumza na wananchi wa Mwanga mkoani Kilimanjaro, katika mkutano wake wa kampeni za urais.
Hatua ya ujenzi wa soko hilo kwa mujibu wa Dkt Samia, inachochewa na eneo hilo kuwa na wakulima wengi wa mpunga, mahindi na maharage, lakini wamekosa soko.
Kutokana na kukosekana kwa soko, ameeleza wakulima hao hawafaidiki na shughuli zao, hivyo anacholenga ni kuhakikisha wananufaika.
“Niwaambie ndugu zangu, kwamba tunakuja kujenga soko. Soko kubwa soko la kisasa,” amesema.
Ujenzi wa mradi huo, utaambatana na soko lingine katika Kata ya Kileo, ili kuwaepusha wakulima wa eneo hilo na kuuza bidhaa zao kwa walanguzi.




