Hatima ya Kocha Mkuu wa Simba SC, Fadlu Davids, inaelezwa kufikia mwisho baada ya taarifa kuibuka kwamba amesafiri moja kwa moja kuelekea Morocco kujiunga na Raja Casablanca kama kocha mkuu mpya.
Davids, raia wa Afrika Kusini, amewahi kuwa kocha msaidizi wa Raja Athletic Club msimu juzi kabla ya kutua Simba. Safari yake ya sasa inatajwa kuwa ya kurejea rasmi klabuni hapo kuchukua nafasi ya Lassaad Chabbi, aliyefutwa kazi Jumamosi iliyopita kutokana na mwenendo mbovu wa kikosi hicho.
Simba SC imerejea nchini ikitoka Botswana baada ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Gaborone United kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini kocha huyo hakusafiri na kikosi, akiripotiwa kuunganisha ndege moja kwa moja kwenda Morocco.
Iwapo tetesi hizi zitathibitishwa, Simba italazimika kuanza safari ya kutafuta kocha mkuu mpya mapema msimu huu, jambo linaloweza kuibua changamoto kwa maandalizi ya timu kuelekea hatua za makundi ya Ligi ya Mabingwa.