Familia na marafiki wa mwanariadha wa Kenya wanasema wameshtuka baada ya kujua kuwa mtoto wao amekamatwa nchini Ukraine.
Vikosi vya Ukraine vilitoa video ya Evans Kibet, ambao wanasema alikuwa anapigana kwa niaba ya vikosi vya Urusi.
Katika rekodi ya video, mwanariadha anadai kwamba alidanganywa kujiunga na jeshi la Urusi wakati ametembelea nchi hiyo kama mtalii.
Evans Kibet anasema safari yake ya St. Petersburg iliandaliwa na wakala wa michezo na kufadhiliwa na serikali ya Urusi.
Aliiambia vikosi vya Ukraine kwamba mwishoni mwa safari yake, pasipoti yake na simu zilichukuliwa, na alilazimishwa kusaini hati zilizoandikwa kwa Kirusi, bila kujua alikuwa akisajiliwa kama mwanajeshi.
Baada ya wiki ya mafunzo ya kimsingi na kukabidhiwa bunduki, Kibet anasema alikataa kupigana.
Akatoroka na kujificha msituni kwa siku mbili, kabla ya kujisalimisha kwa wanajeshi wa Ukraine.
Katika video iliyotolewa na Ukraine anasihi asirudishwe Urusi akihofia maisha yake.
Serikali ya Urusi bado haijasema lolote kuhusiana na tukio hilo.