Hospitali ya Halmashauri ya Mji Handeni, kwa kushirikiana na Shirika lisilo la Kiserikali la Jhpiego na Pfizer Foundation, imezindua rasmi zoezi la uchunguzi wa awali wa saratani ya matiti kwa wanawake, likiwa na lengo la kupunguza vifo vinavyosababishwa na ugonjwa huo nchini.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo, Dkt. Hudi Muradi, aliwataka wakazi wa Handeni kujitokeza kwa wingi kufanya uchunguzi wa saratani ya matiti, akisisitiza kuwa ugunduzi wa mapema ni hatua muhimu katika kuokoa maisha na kupunguza madhara makubwa yanayotokana na kuchelewa kutambua ugonjwa huo.

“Wananchi wanapaswa kuelewa kuwa saratani ya matiti ikigunduliwa mapema, inatibika. Tunawahimiza wanawake wote kutumia fursa hii muhimu kufanya uchunguzi bure,” alisema Dkt. Muradi.

Kwa upande wake, Dkt. Rashid kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga – Bombo, alitoa elimu kuhusu dalili na viashiria vya awali vya saratani ya matiti, akihimiza jamii kuwa na uelewa mpana kuhusu afya ya matiti na umuhimu wa uchunguzi wa mara kwa mara.
Naye Dkt. Laurence Loitore kutoka Hospitali ya Halmashauri ya Mji Handeni, aliishukuru Jhpiego kwa kutoa mafunzo ya kitaalamu kwa wahudumu wa afya, akisema hatua hiyo itasaidia kuongeza uwezo wa wataalamu hao katika kutoa huduma za uchunguzi wa saratani kwenye vituo vyote vya afya vilivyo chini ya Halmashauri.
Zoezi hilo ni sehemu ya juhudi za Serikali kwa kushirikiana na wadau wa afya katika kupambana na vifo vinavyotokana na saratani ya matiti, sambamba na kuimarisha huduma za uchunguzi, kinga, na matibabu kwa wanawake nchini.





