Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Handeni, Maryam Ukwaju amesema mradi wa jengo la wagonjwa Mahututi katika Hospitali ya Halmashauri hiyo litakapokamilika litaondoa adha kwa wananchi kusafiri takribani kilomita 160 kufuata huduma hizo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga.
Akisoma taarifa ya mradi huo kwa Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, akiwa katika ziara yake ya kikazi wilayani Handeni, Ukwaju amesema uwepo wa jengo hilo ni juhudi za Serikali katika kuboresha huduma za afya na kuwataka watendaji kuhakikisha miundombinu hiyo inatumika ipasavyo kuokoa maisha ya wananchi.
“Uwepo wa ICU hii utaondoa changamoto iliyokuwa inawakabili wagonjwa mahututi waliolazimika kusafirishwa umbali mrefu kupata huduma, hali iliyokuwa ikiongeza hatari kwa maisha yao pamoja na gharama kwa familia,” amesema.

Awali, amefafanua kuwa Mradi wa ujenzi wa jengo la ICU ulianza Mei 6, 2024 na kukamilika Mei 25, 2025 kwa gharama ya zaidi ya Sh. milioni 426, ukitekelezwa na kampuni ya SWASH Construction Co. Limited kwa kushirikiana na CAREMED Gas Limited waliotekeleza mfumo wa gesi ya oksijeni.
Amesema Halmashauri tayari imelipia vifaa tiba vya awali vyenye thamani ya Sh. milioni 200 kupitia Bohari ya Dawa (MSD), huku ununuzi wa vifaa tiba vingine pamoja na awamu ya pili ya mfumo wa gesi ya oksijeni ukitarajiwa kutekelezwa katika mwaka wa fedha 2026/2027.
Ujenzi wa jengo hilo ni sehemu ya maboresho ya miundombinu ya afya yaliyowezeshwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambapo alitoa Sh. milioni 900 kwa awamu ya pili kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa majengo mbalimbali ya hospitali hiyo.
Nao, wananchi wa Handeni wameeleza matumaini yao kuwa kuanza kwa huduma za ICU kutasaidia kuokoa maisha ya wagonjwa wengi, kuongeza ufanisi wa huduma za afya na kupunguza msongamano katika hospitali za rufaa za mkoa.





