Wednesday, March 4, 2026
spot_img
HomeHabariKapinga aahidi ushirikiano Mkako, Kihangimahuka

Kapinga aahidi ushirikiano Mkako, Kihangimahuka

Mbunge wa Mbinga Vijijini na Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, ameendelea na ziara yake katika Kata za Mkako na Kihangimahuka kwa lengo la kuwashukuru wananchi kwa ushindi mkubwa waliompatia yeye pamoja na Rais Samia Suluhu Hassan, katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Lihale,  Kapinga amesisitiza dhamira yake ya kuendelea kushirikiana kwa karibu na Serikali ya Wilaya pamoja na taasisi mbalimbali za umma katika kutatua changamoto zinazowakabili wananchi, hususan katika sekta za miundombinu, maji na umeme.

“Serikali ipo pamoja nanyi, na mimi kama Mbunge wenu nitaendelea kushirikiana na viongozi wa wilaya na taasisi zote kuhakikisha changamoto zenu zinapatiwa ufumbuzi wa kudumu,” amesema Kapinga.

Katika kuunga mkono maendeleo ya sekta ya elimu, Kapinga ametoa msaada wa bati 50 za geji 28 zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 1.7 pamoja na shilingi laki tano kwa ajili ya ununuzi wa kenchi, kwa ajili ya ujenzi wa chumba kimoja cha darasa katika Shule ya Msingi Lihale.

Aidha, ametembelea Shule ya Sekondari Kihangimahuka ambako alikabidhi kompyuta moja yenye thamani ya shilingi milioni 2.5 pamoja na mifuko 50 ya saruji yenye thamani ya shilingi laki tisa, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji. Vilevile, aliahidi kuipatia shule hiyo mashine ya fotokopi kabla ya kumalizika kwa mwezi Februari 2026.

Kwa upande wake, mwakilishi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga Vijijini amesema Serikali itaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika jimbo hilo, hususan katika sekta ya afya. Alieleza kuwa jumla ya wahudumu wa afya 100 wameanza kuwasili katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri, wakiwemo madaktari zaidi ya 10, manesi wenye shahada zaidi ya 30 pamoja na wataalamu wengine wa afya.

Mwakilishi huyo amempongeza Kapinga kwa mchango wake katika kuboresha huduma za afya, ikiwemo kusaidia upatikanaji wa gari la wagonjwa (ambulance) ambalo limekuwa msaada mkubwa kwa wananchi, pamoja na ahadi yake ya kukarabati jengo la kinamama katika Zahanati ya Lihale.

Kwa upande wao, wananchi wa Kata za Mkako na Kihangimahuka walimpongeza na kumshukuru Mbunge wao kwa michango yake binafsi katika miradi ya maendeleo, wakieleza kuwa hatua hizo zimeongeza mshikamano na hamasa ya wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya jamii.

Ziara hiyo ni sehemu ya mkakati wa Mbunge huyo wa kuimarisha ushirikiano kati ya wananchi, viongozi na taasisi za serikali, kwa lengo la kufanikisha maendeleo endelevu katika Jimbo la Mbinga Vijijini.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments