Thursday, December 18, 2025
spot_img
HomeHabariKatibu Mkuu Wizara ya Maji akagua marekebisho ya Mtambo wa Maji Butimba

Katibu Mkuu Wizara ya Maji akagua marekebisho ya Mtambo wa Maji Butimba

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri, amefanya ziara katika mradi wa maji wa Butimba, mkoani Mwanza, kufuatilia kazi za marekebisho yanayoendelea baada ya mtambo wa kusukuma maji kupata hitilafu iliyosababisha usumbufu wa upatikanaji wa huduma hiyo kwa wananchi.

Mhandisi Mwajuma, akiwa ameongozana na wataalam wa wizara pamoja na wahandisi wa mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira, alishiriki moja kwa moja katika jitihada za kurekebisha hitilafu hiyo kwa saa 24 mfululizo, akisisitiza dhamira ya serikali kuhakikisha wananchi wanapata maji bila usumbufu.

Amesema serikali imewekeza fedha nyingi katika mradi wa maji wa Butimba kwa lengo la kupunguza changamoto ya upatikanaji wa maji katika Jiji la Mwanza na maeneo jirani, hivyo ni wajibu wa wataalamu kuhakikisha miundombinu inasimamiwa kwa umakini na huduma inapatikana muda wote.

“Lengo letu ni kuhakikisha wananchi wanapata maji ya kutosha muda wote. Hii ni dhamira ya serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuboresha huduma za kijamii, ikiwemo maji safi na salama,” alisema Mhandisi Mwajuma.

Aidha, aliwahakikishia wananchi kuwa hitilafu hiyo ilikuwa ya muda mfupi na hatua zinazochukuliwa zitarejesha huduma ya maji katika hali ya kawaida ndani ya muda mfupi. Alitoa wito kwa wananchi kuendelea kuwa na subira na kushirikiana na mamlaka husika wakati marekebisho yakikamilika.

Mradi wa maji wa Butimba ni miongoni mwa miradi mikubwa ya kimkakati inayotekelezwa na serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo, ukiwa na lengo la kuongeza upatikanaji wa maji safi kwa maelfu ya wakazi wa Jiji la Mwanza na vitongoji vyake.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments