Kayombo-Jitokezeni kwa wingi kujiandikisha katika daftari la wapiga kura

MSIMAMIZI wa Uchaguzi Jimbo la Arusha Mjini John Kayombo ametoa wito kwa wananchi wa jimbo hilo, wenye umri wa miaka 18 na kuendelea, kujitokeza kwa wingi kwenye zoezi la kujiandikisha katika daftari la wapiga kura, ambalo litafanyika kuanzia Oktoba 11 hadi Oktoba 20 kwenye vituo vilivyopangwa.

Aidha msimamizi huyo amewahamasisha  wananchi wenye sifa za kugombea nafasi mbalimbali ikiwa ni pamoja na wenye umri wa miaka 21 na kuendelea, kujitokeza katika uchaguzi huo,  kwa wingi kwa kuwa ni haki ya kisheria.

Kayombo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, alisema hayo leo, wakati akitoa maelekezo ya uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27 mwaka huu.

Kwa mujibu wa Kayombo fomu za kugombea nafasi ya mwenyekiti wa Mtaa,kitongoji na wajumbe wa halmashauri ya kijiji, fomu zitatolewa na kutakiwa kurudishwa kuanzia Novemba Mosi hadi Novemba saba mwaka huu kwa msimamizi wa uchaguzi.

“Uteuzi wa wagombea wote utafanyika Novemba nane mwaka huu na muda wa  kuweka pingamizi kuhusu uteuzi wa wagombea hao, ni kuanzia Novemba 8 hadi 9 mwaka huu na uamuzi wa pingamizi utatolewa kuanzia Novemba 8 hadi 10 mwaka huu,”amesema.

Aidha amesema rufaa dhidi uamuzi kuhusu pingamizi la uteuzi zitapokelewa kuanzia Novemba 10 hadi 13 mwaka huu na kamati ya rufaa itatolewa kuanzia Novemba 10 hadi 13 mwaka huu.

Amesema kampeni za uchaguzi zitaanza Novemba 20 hadi 26 mwaka huu, kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 12:00 jioni.

Msimamizi huyo ametoa wito kwa wananchi wote wenye sifa kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uchaguzi huo, kuanzia hatua ya kujiandikisha kwenye orodha ta wapiga kura kwani ni hatua muhimu inayompa kila mwananchi mwenye sifa haki ya kisheria, kushiriki uchaguzi kama mpiga kura au mgombea

“Hivyo wananchi tunawahimiza kujitokeza kwa wingi kujiandikisha ili kutumia haki yao ya kupiga kura au kugombea nafasi za uongozi na nafasi zitakazogombewa katika uchaguzi huo ni mwenyekiti wa mtaa,wajumbe watano ambao kati yao wajumbe wawili ni wanawake,”amesema.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *