Monday, December 15, 2025
spot_img
HomeBiasharaKituo cha kwanza cha rejareja cha gesi asilia (CNG) chazinduliwa Dar

Kituo cha kwanza cha rejareja cha gesi asilia (CNG) chazinduliwa Dar

Dar es Salaam imeandika historia mpya leo baada ya kuzinduliwa kituo cha kwanza cha rejareja cha Gesi Asilia iliyoshindikizwa (CNG), kilichojengwa eneo la Tangi Bovu, Barabara ya Bagamoyo. Uwekezaji huo unaifanya kampuni inayosimamia mradi huu kuwa kinara wa kuleta suluhu za kisasa za nishati nchini.

Uzinduzi huo ulihudhuriwa na Mgeni Rasmi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Eng. Felchesmi J. Mramba, pamoja na viongozi wengine akiwemo Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Bi. Fatma M. Abdallah, Kaimu Balozi wa Canada, Bi. Carol Mundle, na viongozi waandamizi wa kampuni.

Kituo hicho kipya kimejengwa kwa teknolojia ya kisasa kikiwa na uwezo wa kuzalisha gesi milioni moja za futi za ujazo kwa siku na kuhudumia magari madogo, makubwa na bajaji. Kina mashine mbili zenye uwezo wa kuhudumia magari 50 kwa saa, compressor kutoka Canada yenye nguvu ya 250 HP (1,200 Sm³/hr), pamoja na hifadhi ya gesi ya lita 4,000 inayohakikisha huduma bila kukatika hata wakati wa mahitaji makubwa. Aidha, kituo kimewekewa mfumo wa ukaguzi wa ubora wa gesi ili kuhakikisha usalama na ufanisi.

Mbali na huduma ya CNG, kituo hicho pia kinatoa huduma za petroli, dizeli, LPG, vilainishi pamoja na duka dogo, na hivyo kuwa kituo cha huduma kamili kwa madereva na wafanyabiashara.

Akizungumza katika hafla hiyo, Bi. Fatma M. Abdallah alisema:
“Uzinduzi wa kituo hiki cha CNG ni hatua mpya kwa kampuni yetu nchini Tanzania. Tuna furaha kuanzisha miundombinu ya kisasa inayosaidia kupunguza uzalishaji wa hewa ya kaboni na kutoa huduma ya uhakika kwa wateja. Muhimu zaidi, huu ni mwanzo—tuko tayari kufungua vituo zaidi kabla ya mwisho wa mwaka huu.”

Naye Mkuu wa Kitengo cha Sheria na Masuala ya Kampuni, Bw. Emmanuel G. Bakilana, aliongeza:
“Wateja wetu wanaweza kuitegemea kampuni yetu kwa usalama, ubora na upatikanaji wa uhakika. Kituo hiki kinaonyesha dhamira yetu ya kuwekeza katika miundombinu ya kisasa na kuthibitisha nafasi yetu kama kinara wa suluhu rafiki za usafirishaji.”

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments