Thursday, December 18, 2025
spot_img
HomeMichezoKocha JKT Tanzania avutiwa na Valentino

Kocha JKT Tanzania avutiwa na Valentino

Kocha Mkuu wa JKT Tanzania, Ahmad Ally, ameonesha kuvutiwa na uwezo wa straika kijana Valentino Mashaka, akisema ana nafasi ya kufanya makubwa msimu huu endapo ataweka akili yake kwenye soka na kujituma ipasavyo.

Valentino amejiunga na JKT Tanzania kwa mkopo wa mwaka mmoja akitokea Simba SC, baada ya kushindwa kupata nafasi ya kutosha ya kucheza katika kikosi cha mabingwa hao wa kihistoria.

“Valentino ametoka Simba, klabu kubwa iliyomnyima nafasi ya mara kwa mara, lakini hapa JKT Tanzania atapata nafasi ya kucheza. Ni jukumu lake kuondoa mawazo ya kwa nini ameondoka kule na kuzingatia kazi yake. Soka haina makao maalum, ni kama mtu anayeishi nyumba za kupanga,” alisema Ahmad.

Kocha huyo alisema straika huyo, ambaye msimu uliopita alifunga mabao mawili kwenye Ligi Kuu Bara, bado ana umri mdogo na muda mrefu wa kupiga hatua kubwa katika soka.

“Umri unamruhusu. Kila mechi atakayopata nafasi anatakiwa aonyeshe uwezo wake. Nikiangalia mazoezini ninaona kabisa ana kipaji cha kufika mbali sana. Kazi yangu ni kuhakikisha kila mchezaji anapewa mbinu na motisha ya kufanikiwa,” alisema.

Valentino alijiunga na Simba akitokea Geita Gold kabla ya kutolewa kwa mkopo. Sambamba naye, JKT pia imempokea Salehe Karabaka kwa makubaliano na Simba, huku klabu hiyo ya Msimbazi ikiwachukua moja kwa moja kipa Yakoub Suleiman na beki wa kati Wilson Nangu.

Valentino na Karabaka wanatarajiwa kuanza kuonekana uwanjani leo, wakati JKT Tanzania ikianza msimu mpya wa Ligi Kuu kwa kuvaana na Mashujaa FC katika Uwanja wa Lake Tanganyika.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments