Kocha wa makipa wa JKT Tanzania, Fatuma Omary, amesema anajivunia kuwa miongoni mwa makocha wanaotoa magolikipa wenye ubora wa kimataifa nchini.
Miongoni mwa wachezaji waliopitia mikononi mwake ni Yaqoub Suleiman, kipa wa kwanza wa Taifa Stars na Simba SC baada ya majeraha ya Moussa Camara.
“Najivunia kuona makipa niliowafundisha wanafika mbali hadi kuichezea Timu ya Taifa. Hilo hunipa nguvu zaidi ya kuendelea kuinua vipaji vya vijana,” alisema Fatuma, ambaye aliwahi kuwa kipa wa Twiga Stars.
Amesema lengo lake ni kuendeleza vipaji vya vijana na yupo tayari kumfundisha kijana yeyote mwenye ndoto ya kuwa kipa bora.
“Tanzania ina vipaji vingi, endapo vijana watapata mafunzo sahihi tutazalisha magolikipa wa viwango vya juu duniani,” aliongeza.
Katika mchezo wao wa Ligi Kuu dhidi ya Simba SC uliomalizika kwa kipigo cha 2–1, kipa Gonzo wa JKT aliwavutia mashabiki kwa kuokoa hatari kadhaa langoni.
Kwa sasa, JKT Tanzania inashika nafasi ya saba kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi saba, baada ya kushinda mechi moja, sare nne na kupoteza moja.




