Mmoja wa wamiliki wa eneo la ufukwe wa Coco jijini Dar es Salaam, Bw. Richard Machangu, amemuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, kuingilia kati ili kumsaidia kupata vibali vya kuwekeza katika eneo lake, akidai kuwa juhudi zake zimekuwa zikikwamishwa kwa muda mrefu bila sababu za msingi.
Akizungumza na waandishi wa habari akiwa ufukweni hapo, Machangu alisema ana nyaraka zote halali za umiliki wa eneo hilo tangu mwaka 1992, lenye ukubwa wa zaidi ya hekari 10, lakini kila anapoomba kibali cha kuendeleza eneo lake hukutana na visingizio visivyo na msingi, vikiwemo madai ya kutakiwa kupewa eneo lingine analosema halijui.
“Ni zaidi ya miongo mitatu sasa tunamiliki eneo hili kihalali na tumekuwa tukilipa kodi, lakini kila tunapotaka kuwekeza tunakutana na vikwazo visivyoelezeka. Harufu ya njama za wachache kunyang’anya eneo hili ni kubwa, ndiyo maana naomba msaada wa Mheshimiwa Rais Samia,” alisema Machangu.
Kwa upande wake, wakili wa Machangu, Bw. Sweetbert Nkuba, alisema mteja wake ameagiza suala hili lifuatiliwe kwa kina na iwapo haki haitapatikana, wako tayari kulipeleka mahakamani.
“Mteja wangu amekuwa analipa kodi ya ardhi inayozidi shilingi milioni 30, lakini bado anawekewa vikwazo. Ni wazi kwamba kuna watu wachache wanaojaribu kumzuia kwa maslahi binafsi. Haki hii italindwa kwa mujibu wa sheria,” alisema Nkuba.
Machangu alisisitiza kuwa lengo lake ni kuwekeza katika eneo hilo kwa ajili ya maendeleo ya jamii na kukuza uchumi, hivyo anatarajia mamlaka husika kushughulikia jambo hilo kwa haraka na haki.




