KITUO cha Ubia Kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPPC), kimesema mwisho mwa mwezi huu kitatuma wataalam kwenda Manispaa ya Ilemela jijini Mwanza, kwa ajili ya kuangalia maeneo muhimu ya miradi ya ubia.

Uamuzi huo umekuja baada ya madiwani wa Manispaa ya Ilemela kutembelea PPPC jana kujifunza namna kinavyofanyakazi na watakavyotumia raslimali ardhi waliyonayo kutekeleza miradi ya ubia baina ya sekta binafsi na sekta ya umma.
Mkurugenzi Mkuu wa PPPC, David Kafulila ameyasema hayo leo (Januari 8,2024), wakati akizungumza na madiwani wa Manispaa hiyo ambao pia mionhoni mwao alikuwepo Mbunge wa Jimbo la Ilemela,Angelina Mabula,Meya wa Ilemela, Renatus Mulunga,na Mwenyekiti wa CCM,Yusuph Bujiku.
Amesema uamuzi wa Manispaa hiyo ni mzuri sana kwa kuwa wataendesha miradi kwa kutumia mtaji wa umma ambao unapatika kwa ubia na sekta binafsi.
“Mmefanya uamuzi sahihi kuja kututembelea,mjifunze kwa kuona mradi wetu wa DDC ambao unatekelezwa kwa PPP ila tuna miradi mingine iliyopo katika hatua mbalimbali 82,mna maeneo mengi ambayo mnaweza kuyaendeleza kwa mtaji wa umma,”amesema.
Kafulila amesema ubia ni ndoa ya ushirikiano na si ubinafsishaji kama inavyoelezwa na kwmaba miradi ya ubia yote ni mali ya serikali kabla,wakayi na baada ila sekta binafsi inaingiza mtaji na kuendeleza.
Aidha,amezitaja sababu za ubia kuwa ni kuvuna mtaji wa sekta binafsi kwa ajili ya kutekeleza miradi ya serikali badala ya kukopa,na kwamba fedha ambayo serikali inge tumia kuwekeza itatekeleza miradi mingine maeneo ambayo sekta binafsi haijaona fursa.


“Sekta binafsi inaweza isivutiwe kujenga hospitali au barabara eneo la kijijini kwasababu watu ni wachache ila ikavutiwa kujenga mjini ambako kuna watu.Wanawekeza mtaji mahali ambako wanajua utarudi,hivyo Ilemela ni eneo sahihi kwa uwekezaji wa PPP,”amesema.
Amezitaja sababu nyingine za uwekezaji kuwa ni kuvuta mitaji kutoka sekta binafsi,kuvuta tekonolojia ambayo utafiti unaonyesha in sekta binafsi imepiga hatua eneo hilo.
Nyingine ni kuongeze ufanisi wa kiutendaji kwa kiwa sekta binafsi inamudu kusimamia mambo yake kwa ufanisi mkubwa bila uranium kuliko ambayo serikali inge fanya.
Nyingine ni uamuzi wa kiufanisi,huku akitolea mfano kuwa zipo sekta binafsi huajiri wakurugenzi wa mshahara mkubwa kwa kuwa wanachokitafuta ni ufanisi,hivyo kwa PPP sekta binafsi inaweza kununua mtaalam mwenye ufanisi mkubwa kwenye utekelezaji wa miradi.
Kwa mujibu wa Kafulila,mahitaji ya binadamu yanaongezeka kila siku kuliko uwezo wa serikali yoyote duniani kuyamudu,na kwamba chanzo cha mapato cha serikali ni kodi na mikopo,hivyo haiwezi kumudu kuyatimiza bila PPP.
“Uzoefu unaonyesha kuwa serikali haiwezi kufikia matarajio kwasababu inategemea kodi na mikopo.Deni la dunia kwasasa ni dola trillion 300 huku uchumi ukiwa ni Dola trillion 110 ambayo ni mara tatu ya uchumi,”


“Deni hili ni la serikali,sekta binafsi na kaya…hii inaonyesha kuwa hatuwezi kukwepa kushirikiana na sekta binafsi kutekeleza miradi,leo mtu wa Kigoma vijijini atatamani maisha kama ya mtu wa Kigoma mjini,siku akiyapata atataka ya juu zaidi,hivyo mahitaji ya binadamu yanaongezeka kila siku,”amesema.
“Huwezi kutimiza mahitaji kwa kukopa,lazima ualike sekta binafsi ije na mitaji yake itekeleze,kwa kutumia PPP unatekeleza miradi bila kugusa bajeti na kupunguza shinikizo kwenye vitabu vya serikali.Ilemela mmefanya uamuzi sahihi,”alisema Kafulila.
Aidha,alisema michuano ya AFCON 2027 ni fursa kwa Tanzania kutumia PPP kujenga viwanja na huduma nyingine muhimu,na kwamba ni muhimu ikaangaliwa kama fursa ya kiuchumi.
Naye,Meya wa Manispaa ya Ilemela, Renatus Mulunga, amesema wapo tayari kwa kuwa wana maeneo mengi ambayo yanaweza kutumika kutekeleza miradi kwa ubia,na kwamba ndio sababu ya kujifunza ili wafanye maamuzi sahihi anapopatikana mwekezaji.
Mbunge wa Jimbo la Ilemela,Angelina Mabula,amesema Manispaa hiyo ilishatenga maeneo ila haijapata mwekezaji na kwamba wameona PPP ndio njia sahihi.
“Tuna eneo la Mahombolo tunaweza kujenga viwanja hasa kwa ajili ya AFCON,tuna hitaji kituo cha mabasi na soko la kisasa,hii hatuwezi kutekeleza kwa bajeti za manispaa bali kwa PPP,”amesema.