Thursday, December 18, 2025
spot_img
HomeMichezoMashindano ya Magari Afrika kufanyika Morogoro wiki hii

Mashindano ya Magari Afrika kufanyika Morogoro wiki hii

Madereva 23 kutoka mataifa mbalimbali barani Afrika wanatarajiwa kushiriki mashindano ya mbio za magari maarufu kama Mkwawa Rally of Tanzania, yenye umbali wa kilomita 338, yatakayofanyika mkoani Morogoro kuanzia Septemba 19 hadi 21, mwaka huu.

Mashindano haya ni mzunguko wa mwisho wa kuwania ubingwa wa Afrika (African Rally Championship – ARC).

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Morogoro, Msimamizi Mkuu wa mashindano hayo, Dk. Mosi Makau, alisema mashindano haya yatakutanisha madereva kutoka mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, huku pia kukiwa na washiriki wa ndani wanaopigania kombe la kitaifa.

Dk. Makau alifafanua kuwa mashindano ya mwaka huu kwa mara ya kwanza yatafanyika Morogoro, yakihusisha hatua tatu: ya kwanza ikiwa kilomita 20, ya pili kilomita 12 na ya tatu kilomita 30, kila moja ikiwa na mizunguko miwili. Mashindano yatakamilika Septemba 21 katika eneo la TFS Mkundi kwa mzunguko mmoja.

“Ndani ya siku tatu tutakuwa na mashindano yenye umbali wa kilomita 338. Naomba wananchi wa Morogoro na Watanzania kwa ujumla wajitokeze kwa wingi kushuhudia tukio hili kubwa,” alisema.

Aliongeza kuwa mashindano hayo yatakuwa fursa kwa wakazi na wafanyabiashara wadogo kufaidika kiuchumi kutokana na ujio wa wageni wengi kutoka ndani na nje ya nchi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Magari ya Mashindano Tanzania, Satinder Birdi, alisema madereva watakaoshiriki wanatoka Uganda, Rwanda, Burundi pamoja na India. Wote wanatarajiwa kuwasili Morogoro kabla ya kuanza kwa mashindano.

Mwakilishi wa Mkwawa Group, Emmanuel Mhagama, alisisitiza kuwa kampuni hiyo itaendelea kushirikiana na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo katika kukuza michezo nchini, hususan mchezo wa magari.

Aidha, Mwenyekiti wa Mount Uluguru Rally Club, Gwakisa Mahigi, aliahidi usalama wa kutosha kwa mashindano hayo kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama, ikiwemo Jeshi la Polisi, FFU, na Jeshi la Zimamoto.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments