Uongozi wa KMC umethibitisha kocha wake mkuu, Marcio Maximo, atakaa benchi katika mchezo wa Septemba 23, 2025 dhidi ya Singida Black Stars, baada ya kushindwa kufanya hivyo kwenye mechi ya kwanza ya Ligi Kuu dhidi ya Dodoma Jiji kutokana na kuchelewa kwa leseni ya ukocha kutoka TFF.
Katika mchezo huo wa ufunguzi uliofanyika KMC Complex, Maximo alikaa jukwaani huku kikosi chake kikishinda 1-0 kwa bao la Daruweshi Saliboko.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa KMC, Daniel Mwakasungula, alisema changamoto ya leseni sasa imetatuliwa na mashabiki wajiandae kuona maendeleo zaidi kwani kikosi kimejengwa kwa kuzingatia ripoti ya benchi la ufundi.
Maximo, raia wa Brazil, anarejea Tanzania kwa mara ya tatu. Awali aliifundisha Taifa Stars (2006–2010) na kuifikisha CHAN 2009, kisha akainoa Yanga mwaka 2014.