Monday, December 8, 2025
spot_img
HomeBiasharaMchechu: Tumepokea gawio la bilioni 16.5 TPC

Mchechu: Tumepokea gawio la bilioni 16.5 TPC

Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu, amesema uamuzi wa Serikali mwaka 2000 kuuza asilimia 75 ya hisa za kampuni ya Tanga Plantation Company (TPC) kwa sekta binafsi ulikuwa hatua muhimu iliyowezesha mageuzi ya kiutendaji, kiuchumi na kiuongezaji tija kwa taifa, na sasa kampuni hiyo inaiingizia Serikali gawio la Sh bilioni 16.5.

Akizungumza katika maadhimisho ya miaka 25 ya ubia kati ya Serikali na TPC yaliyofanyika Moshi, mkoani Kilimanjaro, Mchechu pia alishuhudia uwekaji wa jiwe la msingi la mradi mpya wa kimkakati wa kiwanda cha kuchakata molases (TPC Distillery), unaojengwa kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 52, sawa na Sh bilioni 130.

Uzalishaji wa Sukari Waongezeka Maradufu

Kwa mujibu wake, tangu kuanzishwa kwa ubia huo, TPC imeongeza uzalishaji wa sukari kutoka tani 36,000 mwaka 2000 hadi kufikia tani 120,000 kwa sasa, jambo linaloonyesha ufanisi wa usimamizi na uwekezaji.

Aidha, mwaka 2023 pekee, Serikali ilipokea gawio la Sh bilioni 16.5, huku TPC ikichangia zaidi ya Sh bilioni 75 kwenye mapato ya Serikali kupitia kodi mbalimbali.

“Uwekezaji huu umetupa maslahi makubwa. Mbali na gawio la Sh16.5 bilioni, TPC inachangia zaidi ya Sh75 bilioni kwenye mapato ya Serikali—kiwango kinachoonyesha ufanisi wake na tija ya ubia huu,” alisema Mchechu.

Ajira Zaidi ya 4,000 na Uwekezaji wa Miundombinu

Mchechu alisema TPC imeendelea kuwa mfano bora wa ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi, ikiwa imewezesha ajira zaidi ya 4,000 za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja, sambamba na kuwekeza katika elimu, afya na miundombinu ya jamii.

Aliongeza kuwa zaidi ya Sh bilioni 265 zimeshatumika kuboresha miundombinu, mashamba na teknolojia, hatua iliyowezesha kampuni hiyo kufikia uzalishaji wa wastani wa tani 150 za miwa kwa hekta—kigezo kinachotambuliwa kuwa kati ya bora Afrika.

Ubia Mpya na Uwekezaji wa Kimataifa

Kuhusu mradi mpya wa TPC Distillery, Mchechu alisema ubia huo sasa unamilikiwa kwa asilimia 85 na Serikali pamoja na TPC, huku mwekezaji mpya kutoka nje ya nchi, Isautier Drinks Africa, akimiliki asilimia 15.

Amesema hatua hiyo inaakisi kuongezeka kwa imani ya wawekezaji wa kimataifa katika uthabiti na mvuto wa uchumi wa Tanzania.

Wawekezaji Watoa Kauli

Mwenyekiti wa Miwa Group, Arnaud Lagesse, alisema safari ya miaka 25 ya TPC ni ushahidi wa maono, ustahimilivu na kazi ya pamoja kati ya wadau wote.

Amesema licha ya changamoto za ukame, misukosuko ya soko na mabadiliko ya kiuchumi, kampuni imeweza kuongeza uzalishaji na kufikia rekodi mpya mwaka 2025.

Kwa upande wake, alisisitiza kuwa ujenzi wa kiwanda kipya cha kuchakata molases ni sehemu ya mkakati wa kupanua minyororo ya thamani, kuongeza uhimilivu wa mazingira, na kuimarisha uzalishaji katika sekta ya nishati na viwanda.

Serikali ya Mkoa Yapongeza

Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro, Kiseo Nzowa, aliipongeza TPC kwa mchango wake katika uchumi wa mkoa, hasa kupitia mradi wa TPC Distillery ambao aliutaja kuwa kielelezo cha uwekezaji endelevu.

“Mradi huu una faida kubwa kwani utaongeza ajira mpya, mapato ya Serikali kupitia kodi, kuongeza thamani katika sekta ya sukari na nishati, na kuimarisha ushindani wa Tanzania katika soko la kikanda,” alisema Nzowa.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments