Monday, December 8, 2025
spot_img
HomeBiasharaMfuko wa pamoja wazinduliwa: Uwekezaji usio na hasara

Mfuko wa pamoja wazinduliwa: Uwekezaji usio na hasara

Watanzania wameshauriwa kuchangamkia fursa zilizopo katika uwekezaji kupitia masoko ya mitaji hapa nchini.

Ushauri huo umetolewa na Mkurugenzi wa Utafiti, Sera na Mipango kutoka Mamlaka ya Mitaji na Dhamana, Alfred Mkondo, wakati akizindua mfuko wa kwanza wa uwekezaji wa pamoja kwenye kampuni zaidi ya 12 ambayo yameorodheshwa katika masoko ya hisa ya Afrika Mashariki.

Mkondo amesema mfuko huo ni wa pekee kwa sababu unapunguza uwezekano wa kupata hasara na kwamba unatoa fursa kwa mwananchi kupata faida.

Amesema pia unatoa fursa kwa mwananchi kuwekeza katika dhamana zaidi ya moja na kwamba lengo lake ni kumwezesha mwananchi kupata faida zaidi.

“Kama ukiwekeza katika dhamana moja au dhamana mbalimbali, utakuwezesha kupata faida hata kama kampuni moja itapata hasara, ni uwekezaji wa kibunifu ambao utakuwa ni mfuko wa kwanza wa aina hiyo katika soko letu la hisa la Dar es Salaam,”amesema Mkondo.

“Niwasihi Watanzania tuchangamkie fursa kama hizi ambazo zinajitokeza katika masoko ya mitaji hapa nchini, tusiwe na uwekezaji mmoja tu wa mashamba, daladala, bali wekeza kila aina ili zinapotokea fursa katika eneo fulani za masoko na wewe unufaike, tusipende kuachia nafasi na tungependa Watanzania wengi wanufaike kupitia fursa zinazopatikana katika masoko ya mitaji.”

Amesema ni vema Watanzania wakajenga utamaduni wa kuwekeza katika mifuko ya namna hiyo kwa sababu inasimamiwa na kuangaliwa uwezo wake na wataalamu waliothibitishwa na hivyo kupunguza vihatarishi vya kupata hasara.

Mkurugenzi wa Kampuni ya kifedha ya iTrust, Mohammed Wasame, amesema mwananchi atakayepata nafasi ya kuwekeza katika mfuko huo, atapata fursa ya kupata faida kutoka katika nchi zote ambazo zimeorodheshwa katika soko la hisa.

Pia, amesema katika mfuko huo mpya wa uwekezaji, wamepunguza kiwango cha kuanzia cha uwekezaji na sasa kitaanzia Sh.100,000 ili kutoa fursa kwa wananchi wengi kuwekeza na kunufaika na mfumo huo mpya wa uwekezaji katika kampuni kubwa Afrika Mashariki.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments