Tuesday, December 16, 2025
spot_img
HomeHabariMgogoro wa ardhi wazua taharuki Bwakila Chini, Morogoro

Mgogoro wa ardhi wazua taharuki Bwakila Chini, Morogoro

Mgogoro wa ardhi umeibua taharuki katika Kijiji cha Bwakila Chini, wilayani Morogoro, baada ya wananchi kufunga ofisi ya kijiji wakipinga kuuza ekari 207 za ardhi kwa kampuni ya Morogoro Sugar.

Wananchi wanasema hawakushirikishwa katika mkataba uliosainiwa mwaka 2018, na kwamba mikutano ya kijiji haijawahi kufanyika kujadili mapato, matumizi pamoja na mustakabali wa mashamba yao. Wameeleza kushangazwa na taarifa kuwa mwekezaji alikabidhiwa eneo hilo mwaka 2021, ilhali wao walijulishwa rasmi mwaka 2025.

“Tunamuomba Rais Samia aingilie kati. Viongozi wa chini wametusaliti. Tunaomba ama aje mwenyewe au amtume Waziri Mkuu, Waziri wa TAMISEMI, Waziri wa Ardhi au Mkuu wa Mkoa aje kutusikiliza kwa kina,” alisema mmoja wa wakazi wa kijiji hicho.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Bwakila Chini, Hemedi Mvunyo, alipoulizwa kwa njia ya simu alikanusha madai hayo. Alisema mikutano ya kijiji hufanyika kila robo mwaka, na kwamba muda si mrefu mkutano mwingine utafanyika ambapo mwekezaji ataalikwa kutoa ufafanuzi mbele ya wananchi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro alieleza kuwa ametoa maelekezo ofisi ya kijiji ifunguliwe na huduma ziendelee kama kawaida. Aidha, alisema tuhuma zinazohusu mkataba huo zinaendelea kuchunguzwa na ofisi yake.

Wakati huohuo, taarifa kutoka kijijini zinasema watu kadhaa wamekamatwa na polisi na kupelekwa mjini Morogoro kwa tuhuma za kushiriki katika kufunga ofisi ya kijiji.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments