Kocha Mkuu wa Namungo FC, Juma Mgunda, amesema tuzo ya Kocha Bora wa Novemba imempa msukumo mpya kuelekea malengo ya kumaliza ligi kwenye nafasi za juu msimu wa 2025/26.
Mgunda alitwaa tuzo hiyo baada ya kuiongoza Namungo kushinda michezo miwili—Dodoma Jiji (2-0) na Mbeya City (1-0)—na kutoka sare ya 1-1 na Azam FC.
Alisema hakutarajia kutangazwa mshindi kwa kuwa alikuwa analenga ushindi wa timu, lakini tuzo hiyo imempa nguvu zaidi.
“Nawashukuru TFF, Bodi ya Ligi na wachezaji wangu. Tuzo hii inanifanya kuongeza bidii zaidi,” alisema Mgunda.
Wakati huo huo, straika Fabrice Ngoy ametwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa Novemba baada ya kufunga mabao mawili na kusaidia timu kuvuna pointi tano katika dakika 188 alizocheza.




