Sunday, November 2, 2025
spot_img
HomeAfyaMradi wa HEET taswira MUHAS kuwa kitovu cha madaktari bingwa

Mradi wa HEET taswira MUHAS kuwa kitovu cha madaktari bingwa

Dar es Salaam, 27 Oktoba 2025 —Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kimesema ujenzi wa Ndaki ya Tiba katika Kampasi ya Mloganzila umefikia asilimia 50, ukiwa sehemu ya utekelezaji wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Uchumi (Higher Education for Economic Transformation – HEET Project) unaofadhiliwa na Benki ya Dunia kwa ushirikiano na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Akizungumza jijini Dar es Salaam katika mkutano maalum na vyombo vya habari,Makamu Mkuu wa MUHAS, Prof. Appolinary Kamuhabwa amesema chuo kimepokea dola za Kimarekani milioni 45.5 (takribani shilingi bilioni 120) kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya kufundishia, kujifunzia, kufanya tafiti, na kuendeleza mitaala ya kisasa ya taaluma za afya.

Kati ya fedha hizo, zaidi ya dola milioni 30.5 zinatumika katika kuendeleza Kampasi ya Mloganzila na ujenzi wa kampasi mpya ya Kigoma, zote zikiwa chini ya usimamizi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia mradi wa HEET.


Miundombinu ya kisasa kuibadilisha Mloganzila

Amesema kuwa ujenzi wa Ndaki ya Tiba katika Kampasi ya Mloganzila ulianza rasmi Desemba 2024 baada ya kukamilika kwa taratibu zote za manunuzi na ushauri wa kitaalamu kwa mujibu wa miongozo ya Benki ya Dunia na Mamlaka ya Manunuzi ya Umma (PPRA).

“Ujenzi huu unatekelezwa na wakandarasi wawili — Mohammedi Builders Ltd na Hainan International Ltd — chini ya usimamizi wa mshauri elekezi ARQES AFRICA, na unatarajiwa kukamilika Juni 2026.”

Miundombinu inayoendelea kujengwa katika ndaki hiyo ni pamoja na:

  • Kumbi za mihadhara zenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 1,400 kwa wakati mmoja,
  • Jengo la utawala lenye ofisi 450,
  • Maabara 21 za kufundishia,
  • Jengo la Anatomia lenye uwezo wa watumiaji 300,
  • Bweni la wanafunzi lenye nafasi za 320,
  • Bwalo la chakula la watumiaji 550,
  • Jengo la Maktaba na TEHAMA lenye uwezo wa 550,
  • Barabara za ndani na uwanja wa mpira wa miguu.

Kwa upande wa Kampasi ya Kigoma, ujenzi ulianza Disemba 2024 na umefikia asilimia 35. Mradi huu unatekelezwa na China Jiangxi International Economic and Technical Cooperation Co. Ltd, chini ya usimamizi wa OGM Consultants. Kampasi hiyo itakuwa na jengo la utawala na taaluma, maabara, maktaba, bweni la wanafunzi, bwalo la chakula, pamoja na miundombinu ya michezo.


Uwekezaji mkubwa zaidi katika historia ya MUHAS

Prof. Kamuhabwa amesema huo ni uwekezaji mkubwa zaidi kuwahi kufanyika katika MUHAS tangu kuanzishwa kwake mwaka 1963 kama shule ya tiba.

“Uwekezaji huu wa serikali kupitia HEET ni wa kihistoria. Unalenga kuongeza uwezo wa chuo katika kutoa wataalamu wa afya wa ngazi mbalimbali, kuboresha mazingira ya kufundishia, na kuongeza ubora wa elimu ya tiba nchini,” Prof. Kamuhabwa

Menejimenti iliongeza kuwa, katika mwaka wa masomo 2025/2026, MUHAS ilipokea zaidi ya waombaji 31,000 wenye sifa za kujiunga na shahada mbalimbali, lakini walioweza kuchaguliwa ni 986 pekee kutokana na changamoto ya ufinyu wa miundombinu.

“Kwa mfano, katika shahada ya udaktari wa binadamu, kati ya waombaji 5,395 wenye sifa, walioweza kuchaguliwa ni 235 tu. Mradi huu utakapokamilika, utapunguza kwa kiasi kikubwa changamoto hii na kuongeza nafasi za udahili wa wanafunzi wa tiba na fani nyingine za afya,” Prof. Kamuhabwa


Manufaa kwa taifa na sekta ya afya

Kupitia mradi huu, MUHAS inatarajia kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya afya nchini, ikiwemo:

  • Kuongeza idadi ya wataalamu wa afya na madaktari bingwa,
  • Kuboresha tafiti za kisayansi na bunifu,
  • Kuanzisha mitaala mipya 23 na kufanya maboresho katika mitaala 83 ya zamani,
  • Kuongeza ajira zaidi ya 300 kwa Watanzania katika hatua za ujenzi na uendeshaji,
  • Kuchochea biashara za ndani kupitia ununuzi wa vifaa na huduma za ujenzi,
  • Kuimarisha ubora wa elimu na kuvutia wanafunzi wa kimataifa,
  • Kuchangia katika utalii wa tiba (medical tourism) na kuongeza mapato ya Taifa.

Prof. Kamuhabwa amesema kwa upande wa Kampasi ya Kigoma, mradi huo unalenga kuanzisha chuo kipya cha afya katika Ukanda wa Magharibi wa Tanzania, eneo lililo na changamoto za kijiografia na upungufu wa wataalamu wa afya.

Kampasi hiyo itasaidia kufundisha wataalamu katika kada zenye upungufu mkubwa kama orthotics, occupational health, anaesthesia, na physiotherapy, sambamba na kuimarisha huduma za afya katika mikoa ya Kigoma, Rukwa, Katavi na Kagera.

“Uwepo wa chuo hiki utasaidia kupunguza rufaa za wagonjwa wanaolazimika kutafuta huduma za kibingwa katika hospitali za Bugando au Benjamin Mkapa, kwani wataalamu watapatikana ndani ya kanda husika,” ilieleza Menejimenti ya MUHAS.


Serikali, Benki ya Dunia na wadau watunukiwa pongezi

MUHAS imeishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika elimu ya juu na sekta ya afya.

“Uwekezaji huu ni sehemu ya maono ya Rais Samia kuhakikisha elimu ya juu inakuwa chachu ya maendeleo ya uchumi wa kisasa unaotegemea maarifa, teknolojia na ubunifu,” Prof. Kamuhabwa

Shukrani pia zimetolewa kwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Benki ya Dunia, viongozi wa mikoa ya Dar es Salaam na Kigoma, pamoja na wakandarasi na washauri elekezi wanaosimamia utekelezaji wa mradi huo kwa weledi.


Kuelekea 2026: Tanzania yenye wataalamu wa kutosha

Mradi wa HEET ulianza rasmi tarehe 13 Juni 2021 na unatarajiwa kukamilika Julai 2026, ukiwa na malengo saba makuu yakiwemo kuboresha miundombinu, mitaala, tafiti, TEHAMA, ushirikiano na sekta binafsi, pamoja na kuimarisha uwezo wa uongozi katika taasisi za elimu ya juu.

Kwa upande wa MUHAS, Menejimenti imesisitiza kuwa kukamilika kwa mradi huu kutakuwa ni hatua kubwa kuelekea dira mpya ya chuo —

“Kutoa mafunzo bunifu ya afya, kufanya tafiti zenye tija, na kutoa huduma bora kwa kutumia teknolojia na ubunifu.”

Kupitia miradi hii, MUHAS inatarajia kuendelea kuwa kitovu cha ubora wa elimu ya tiba na sayansi za afya Afrika Mashariki, na mchango wake utasaidia kuboresha ustawi wa Watanzania kupitia elimu, utafiti na huduma bora za afya.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments