Msimu wa tatu wa Rombo Marathon 2024 umehitimishwa kwa mafanikio makubwa, ukiongozwa na Rais Mstaafu Dk. Jakaya Kikwete, ambaye alihamasisha wanariadha wa Tanzania kutumia maeneo ya Rongai Forest kwa mazoezi, yakiwa na mazingira ya miinuko na misitu ya asili.

Mbio hizo, zilizofanyika Desemba 23, zilihudhuriwa na maelfu ya wakazi wa Rombo, mikoa jirani, na wageni kutoka sehemu mbalimbali kama Dar es Salaam, Mwanza, Dodoma, Mbeya, Tanga, na Zanzibar. Tukio hilo pia lilivutia wageni mashuhuri kama Prof. Mohamed Janabi, Mshauri wa Rais katika masuala ya afya, ambaye alisisitiza umuhimu wa michezo kwa afya bora.
Mwasisi wa mbio hizo, Prof. Adolf Mkenda, ambaye pia ni Waziri wa Elimu na Mbunge wa Rombo, alibainisha kuwa Rombo Marathon mwaka huu imejumuisha zaidi ya wakimbiaji 1,200 na kuvutia zaidi ya wageni 5,000 waliofika Kilimanjaro kwa ajili ya sikukuu.



Fedha zilizokusanywa kupitia mbio hizo zitaelekezwa kwenye upanuzi wa Hospitali Teule ya Huruma, inayojitayarisha kupandishwa hadhi kuwa Hospitali ya Rufani.
Aidha, Prof. Janabi aliwashauri wakazi wa Rombo kuongeza matumizi ya maji kutokana na hali ya hewa ya uwanda wa juu wa Mlima Kilimanjaro, ambayo huathiri mzunguko wa damu.
Rombo Marathon 2024 sio tu mashindano ya mbio bali pia jukwaa la kukuza afya, utalii, na maendeleo ya kijamii.



