Mgombea ubunge aliyepita bila kupingwa wa Jimbo la Ngorongoro kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Yanick Ndoinyo, ameendelea kuomba ridhaa ya wananchi kuelekea uchaguzi wa Oktoba 29, akiahidi kushirikiana na serikali na wananchi kushughulikia changamoto mbalimbali zinazowakabili wakazi wa jimbo hilo.
Katika ziara yake ya kuomba kura na kumuombea kura za kishindo Rais Samia Suluhu Hassan katika kata za Olorieni, Maaloni na Malambo, Ndoinyo amesema kuwa ilani ya CCM imetenga miradi mikubwa ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa barabara ya kilomita 164 kwa kiwango cha lami kutoka Kigongoni, Mto wa Mbu hadi Sale, Ngorongoro.
Ameeleza kuwa katika kipindi cha miaka minne iliyopita, serikali imetumia zaidi ya shilingi bilioni 88 kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo wilayani humo, na kusisitiza kuwa atahakikisha miradi yote iliyosalia inakamilishwa kikamilifu kwa manufaa ya wananchi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ngorongoro, Lucas Olemasiaya, amesema ziara hiyo inalenga kuwaombea kura wagombea wa chama hicho kuanzia ngazi ya urais, ubunge na udiwani kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 30.




