Timu ya Taifa ya Netiboli ya Tanzania inatarajiwa kuingia kambini Zanzibar kuanzia Novemba 20, 2025, kujiandaa kwa mashindano ya Afrika yatakayofanyika Desemba 8–12, mwaka huu nchini Malawi.
Katibu Mkuu wa Chama cha Netiboli Tanzania (CHANETA), Hilda Mwakatobe, amesema kikosi hicho kitakuwa na wachezaji 22 — 12 kutoka Tanzania Bara na wengine kutoka Zanzibar.
“Kwa sasa tunajiandaa kuelekea Zanzibar kwa ajili ya kambi ya maandalizi kuelekea mashindano ya Afrika. Tunaamini kambi hiyo itawaweka wachezaji tayari kupeperusha bendera ya Tanzania,” alisema Mwakatobe.
Aliongeza kuwa safari ya kuelekea Malawi inatarajiwa kuwa kati ya Desemba 3 au 4, huku akiwahakikishia Watanzania kwamba timu hiyo itapambana kutimiza malengo ya kufanya vyema katika michuano hiyo ya kimataifa.
Mwakatobe aliwaomba wadau na Watanzania wote kuwaunga mkono wachezaji hao kwa kuwasaidia mahitaji mbalimbali ili kuhakikisha wanaiwakilisha vyema nchi.
“Mtu yeyote anakaribishwa kuitembelea timu kambini ili kuwapa moyo na ushauri — jambo hili litawajenga zaidi na kuwapa ari ya uzalendo,” alisema.




