Kocha Mkuu wa New King FC, Abdulrahman Mohamed, amesema wanatarajia mchezo mgumu dhidi ya Uhamiaji FC katika Ligi Kuu Zanzibar leo kwenye Uwanja wa Mau A.
Amesema Uhamiaji ni timu yenye uzoefu, lakini New King imejipanga kwa umakini ili kufuta makosa yaliyowagharimu walipotoka sare na Zimamoto kwenye mechi iliyopita.
“Tumeongeza umakini na tumewasoma wapinzani wetu. Tunajua maeneo yao imara na mapungufu yao, tutayatumia kupata ushindi,” alisema.
Kocha huyo aliongeza kuwa watachagua mfumo utakaoendana na mpinzani, huku lengo likiwa kupata matokeo chanya kwenye mechi nne zilizobaki kukamilisha mzunguko wa kwanza.




