Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman, leo amekutana na wavuvi wa Bandari ya Mnarani, Kijiji cha Makangale, Wilaya ya Micheweni, katika muendelezo wa mikutano yake ya kampeni.
Katika mkutano huo uliojaa hamasa, Othman alisikiliza changamoto zinazowakabili wavuvi na kuwasilisha dira yake ya mageuzi makubwa katika sekta ya uvuvi.
Ameahidi kuwa serikali yake itafanya yafuatayo:”
1.Kuboresha miundombinu ya bandari ndogo na masoko ya samaki ili wavuvi wapate sehemu salama na za kisasa kuhifadhia mazao yao.
2.Kutoa mikopo nafuu na zana za kisasa za uvuvi ili kupunguza gharama za uzalishaji na kuongeza kipato cha wavuvi.
3.Kuwekeza katika teknolojia ya usindikaji na hifadhi ya samaki, ili kuongeza thamani ya bidhaa na kufungua fursa za ajira.
4.Kulinda mazingira ya bahari na kudhibiti uvuvi haramu, sambamba na kutoa elimu kwa jamii za wavuvi juu ya utunzaji wa rasilimali.

Wavuvi walipata nafasi ya kueleza matatizo yao, yakiwemo kupanda kwa gharama za vifaa vya uvuvi, uhaba wa masoko ya uhakika, na ukosefu wa hifadhi bora ya samaki.
Mmoja wao, Ali Said Ramadhan, alilalamikia unyanyasaji unaofanyika kwa kisingizio cha uhifadhi wa maeneo ya kuvulia ambapo mara kwa mara nyavu zao hunyang’anywa.
“Tumechoka kunyanyaswa, vifaa vyote tunachukua kwa mikopo, sasa nyavu zikiharibiwa tutalipia nini?” alihoji kwa masikitiko makubwa.
Akijibu hoja hiyo, Othman alisisitiza kwamba sekta ya uvuvi ndiyo uti wa mgongo wa maisha ya wananchi wengi wa visiwani Zanzibar, na serikali yake itahakikisha haki na maslahi ya wavuvi yanalindwa.
“Serikali ya ACT Wazalendo itaweka uvuvi katika kipaumbele cha kwanza, kwa sababu maendeleo ya Zanzibar hayawezi kujengwa bila kumuinua mvuvi. Huu ndio wakati wa mabadiliko ya kweli!”.





