Sunday, December 7, 2025
spot_img
HomeElimuPDPC, OUT kushirikiana kuandaa maofisa ulinzi wa taarifa nchini

PDPC, OUT kushirikiana kuandaa maofisa ulinzi wa taarifa nchini

Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) imeingia makubaliano ya ushirikiano na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) kwa ajili ya kutoa kozi fupi kwa Maofisa Ulinzi wa Taarifa Binafsi (DPO), watakaosaidia kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kuimarisha usimamizi na ulinzi wa taarifa binafsi.

Hafla ya utiaji saini wa makubaliano hayo ilifanyika Novemba 14, 2025 jijini Dar es Salaam, ikiwa na lengo la kuhakikisha taasisi zinazokusanya na kuchakata taarifa binafsi zinatimiza matakwa ya kisheria, ikiwemo kulinda taarifa na kujisajili na PDPC.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa PDPC, Dk. Lameck Mkilia, alisema ulinzi wa taarifa binafsi ni eneo mtambuka linalohitaji ushirikiano wa wadau mbalimbali pamoja na utoaji wa elimu endelevu ili kuhakikisha faragha ya wananchi inalindwa kikamilifu.

Ameeleza kuwa kupitia makubaliano hayo, PDPC na OUT wataandaa pamoja maudhui ya elimu kwa umma, huku wakihakikisha mazingira ya utoaji wa elimu yanakuwa rafiki na yanayokidhi mahitaji ya Watanzania katika zama za kidijitali.

Kwa upande wake, Naibu Makamu Mkuu wa OUT anayeshughulikia Teknolojia za Kujifunzia na Huduma za Mikoa, Prof. Leonard Kweja, amesema kama chuo kinachotumia TEHAMA katika utoaji wa elimu, OUT kina wajibu mkubwa wa kusimamia masuala ya faragha na ulinzi wa taarifa za watumiaji wake.

“Makubaliano haya ni hatua muhimu kwa OUT katika kulinda haki binafsi za watu. Katika dunia ya kidijitali, taarifa potofu zinaweza kuleta madhara makubwa, hivyo ni muhimu kutambua nafasi ya ulinzi wa taarifa katika kulinda jamii na kuchochea uchumi,” alisema Prof. Kweja.

Naye Makamu Mkuu wa OUT, Prof. Alex Makulilo, alisema chuo hicho kitaendelea kuzingatia matakwa ya PDPC kwa kuhakikisha taarifa za wanafunzi na za taasisi zinalindwa kwa mujibu wa sheria.

Ameongeza kuwa OUT imefanikiwa kutekeleza programu zake kwa ufanisi kutokana na mtandao wake mpana nchi nzima, unaowawezesha wananchi kupata elimu bila kulazimika kufika chuoni moja kwa moja.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments