Tuesday, March 3, 2026
spot_img
HomeAfyaPSSSF yakabidhi vifaatiba vyenye thamani ya mil.55 kuboresha afya ya Mama na...

PSSSF yakabidhi vifaatiba vyenye thamani ya mil.55 kuboresha afya ya Mama na Mtoto

Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) umekabidhi msaada wa vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi milioni 55 katika Hospitali ya Manispaa ya Tabora na Kituo cha Afya Kizimkazi, Mkoa wa Kusini Unguja – Zanzibar, ikiwa ni jitihada za kuboresha huduma za uzazi na kuhakikisha mama na mtoto wanajifungua salama.

Msaada huo ulikabidhiwa Desemba 3, 2025, katika maeneo hayo mawili, ambapo PSSSF ilieleza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya kurudisha kwa jamii na kuwekeza katika maisha ya Watanzania, hususan wenye kipato cha chini.

Akitoa shukrani kwa niaba ya Manispaa ya Tabora, Mkurugenzi wake, Dkt. John Pima, aliipongeza PSSSF kwa kujikita katika kuunga mkono juhudi za serikali kupunguza vifo vya mama na mtoto. Amesema uwekezaji huo unaonyesha dhamira ya mfuko huo katika kulisaidia taifa kufikia malengo ya afya bora kwa wote.

Kwa upande wake, Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dkt. Elisha Ndakama, alisema msaada huo utakuwa na mchango mkubwa kwa akina mama wanaojifungua katika hospitali hiyo.

“Katika mwaka wa fedha 2024/25, akina mama 392 walijifungua salama, ambapo watoto 387 walizaliwa wakiwa hai. Kwa msaada huu, tunatarajia idadi ya akina mama watakaopata huduma salama kufikia 500 katika mwaka wa fedha 2025/26,” alisema Dkt. Ndakama.

Huko Unguja, msaada huo ulipokelewa na Mkuu wa Wilaya ya Kusini Unguja, Othman Maulid, ambaye alilisifu PSSSF kwa kurudisha sehemu ya michango ya wanachama kwa jamii na kuunga mkono juhudi za serikali katika kuboresha miundombinu ya afya.
“Hatua hii ya PSSSF ni ya kupongezwa kwa sababu inaakisi dhamira ya kuimarisha ustawi wa wananchi na kutengeneza jamii yenye afya bora,” alisema.

Naye Daktari Dhamana wa Wilaya ya Kusini Unguja (DMO), Mohammed Mtumwa Mnyimbi, alisema vifaa hivyo vitaboresha utoaji wa huduma na kuimarisha ustawi wa wanachama wa PSSSF.

“Vifaa hivi ni muhimu sana katika utoaji wa huduma zetu za kila siku. Tunawahamasisha wadau wengine kuiga mfano wa PSSSF wa kurudisha kwa jamii,” alisema DMO huyo.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments