Rais Dk Samia Suluhu Hassan amesema ameunda Tume ya ndani Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani, ili zitakapoletwa zile za kimataifa zikutane na iliyopo na kupeana taarifa.
Rais Dk Samia ametoa kauli hiyo leo, Alhamisi Novemba 20, 2025 alipozungumza wakati wa uzinduzi wa Tume ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani, Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma.
Hata hivyo, amesema uamuzi wake wa kuiunda tume hiyo umetokana na matakwa ya Sheria ya Tume za Uchunguzi ya 2023 Sura ya 32, inayompa mamlaka hayo.
“Kwenye hili lililotokea, nikaona kabla ya kuletewa tume za nje tuwe na tume yetu wenyewe ndani, ifanye kazi na za nje zikija zitakuja kuzungumza na tume mwenzao ambayo tayari ilishaanza hiyo kazi,” amesema.




