Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, amewataka wakulima wanaotumia maji ya Mto Ruvu kwa shughuli za kilimo wasitishie matumizi hayo kwa muda, hadi mvua zitakapokuwa nyingi, ili kuepuka kuathiri uzalishaji na usambazaji wa maji kwa wananchi wa Dar es Salaam na Pwani.
Wito huo alitoa wakati akifanya ziara ya ukaguzi katika mitambo ya uzalishaji maji ya Ruvu Chini na Ruvu Juu kwa lengo la tathmini ya hali ya upatikanaji wa maji katika chanzo cha mto huo.
“Mabadiliko ya hali ya hewa, hasa ongezeko la joto, yamesababisha kupungua kwa kiwango cha maji hasa sehemu ya Ruvu Chini. Hali hii pia imesababishwa na shughuli zisizo rasmi za kilimo kando-kando ya mto, ambapo watu huanza kulima bila kupata vibali vinavyotakiwa,” alisema Kunenge.




Kunenge aliongeza kuwa, ingawa uzalishaji wa maji katika mtambo wa Ruvu Chini umepungua, bado si kwa kiwango kikubwa, wakati mtambo wa Ruvu Juu ukiendelea kutoa maji kwa kiwango kinachoridhisha.
“Nitoe wito kwa watumiaji wa maji, hasa wanaotumia maji hayo kwa ajili ya kilimo, wasitishie matumizi yao kwa muda hadi mvua zitakaposhuka tena na maji ya mto kuongeza upya. Kwa sasa maji haya yanatakiwa kutumika kwa ajili ya matumizi ya binadamu pekee. Aidha, tutachukua hatua dhidi ya wale wanaotumia maji ya mto kwa kilimo bila vibali na kusababisha changamoto,” alisema.
Aidha, alibainisha kuwa kukamilika kwa ujenzi wa Bwawa la Kidunda kutasaidia kupunguza changamoto ya upungufu wa maji kwa kuhifadhi maji kwa wingi, bila kutegemea mvua za msimu pekee.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri, ametoa wito kwa wanaharakati wa Bonde la Mto Wami-Ruvu kushirikiana na DAWASA kufanya juhudi za haraka na za pamoja kuboresha maeneo yenye changamoto katika mto Ruvu yanayosababisha upotevu wa maji na kupungua kwa wingi wa maji mtoni, ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji salama na endelevu.





