Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umewagawia Watumishi wa Jeshi la Magereza mkoani Shinyanga jumla ya majiko ya gesi yenye sahani mbili pamoja na mitungi ya kilo 15 kwa askari na maafisa 221, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa kusambaza nishati safi nchini.
Hafla ya ugawaji huo ilifanyika Septemba 24, 2025 ambapo Mjumbe wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Mhandisi Ahmed Chinemba, aliwataka askari wa Magereza kuwa mabalozi wa matumizi ya nishati safi katika jamii, akisisitiza kuwa hatua hiyo inalenga kupunguza uharibifu wa mazingira unaosababishwa na ukataji miti kwa ajili ya kuni na mkaa.
Chinemba alisema mpango huo unatokana na mkataba kati ya REA na Jeshi la Magereza uliosainiwa Septemba 2024 wenye thamani ya shilingi bilioni 35, ambapo REA ilichangia shilingi bilioni 26 na Jeshi la Magereza likachangia shilingi bilioni 8. Mradi huo unahusisha ujenzi wa miundombinu ya bayogesi 126, majiko banifu 377, miundombinu ya gesi asilia (LPG) 64 na majiko banifu 256, pamoja na usambazaji wa mitungi ya gesi 15,126 ya kilo 15 na tani 850 za mkaa mbadala (Rafiki briquettes).


“Ninawapongeza Magereza kwa kuwa vinara wa matumizi ya nishati safi, jambo linalokwenda sambamba na agizo la Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwamba taasisi zinazohudumia watu zaidi ya 100 zisitumie tena kuni na mkaa, bali zigeukie nishati safi,” alisema Chinemba.
Kwa upande wake, Mkuu wa Magereza Mkoa wa Shinyanga, Kamishna Msaidizi Mwandamizi Nobert Ntacho, aliishukuru serikali kupitia REA na kueleza kuwa familia za askari na watumishi watanufaika kwa kuwa tayari wamepatiwa mafunzo ya matumizi ya gesi na teknolojia nyingine za nishati safi.
Aidha, Mkuu wa Gereza la Wilaya ya Shinyanga, Kamishna Msaidizi Martin Kunambi, alisema gereza hilo linalohudumia mahabusu 263 tayari limejenga miundombinu ya kupikia kwa kutumia nishati safi, sambamba na agizo la Rais Samia.
“Tunaipongeza na kuishukuru serikali, leo tumepokea majiko na mitungi ya gesi 221 sawa na idadi ya askari na watumishi waliopo hapa mkoani Shinyanga,” alisema Kunambi.
Hatua hii imeelezwa kuwa miongoni mwa mkakati wa serikali wa kuhakikisha taasisi kubwa nchini zinatumia nishati safi, kupunguza uharibifu wa mazingira na kulinda afya za wananchi.








